×

Samia: Longido Kulikuwa na DED Mkorofi, Nilimuondoa – Video

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi kufanya kazi kwa weredi na kuacha malumbano badala yake kusimamia vizuri miradi ya Serikali ili kuwaletea maendeleo Watanzania.

 

Rais Samia amesema hayo leo Jumatatu, Oktoba 18, 2021 wakati akihutubia mara baada ya kuzindua kiwanda cha nyama Eliya Food Overseas LTD kilichopo Eurendeke, wilayani Longido Mkoani Arusha.

 

“Nimekuja Longido kwa madhumuni makubwa matatu, moja kwa kuwashukuru kwa kazi kubwa mlioifanya mwaka jana kwa kukipa kura Chama Cha Mapinduzi, wanasema imani huzaa imani, mmetupa imani nasi tutawalipa imani, pili kuzindua kiwanda cha nyama na mradi wa maji.

 

“Nihimize kufanya kazi kwa nidhamu, hapa Longido kulikuwa na Mkurugenzi mkorofi sana, hakukuwa na nidhamu ndio maana nikamtoa na kumpeleka kwingine akajifunze, ilikuwa nimuache kabisa, niwasisitize wote kuheshimiana na nidhamu ya kazi, kila mtu ana mamlaka yake.

 

“Mbali na mambo yote yanayoletwa na maji kwamba maji ni uhai maji ni maendeleo, lakini maji ni sadaka. Yule aliyetoa billion 15.7 zije Longido ili Longido ipate maji, hatunaye tena. Naye si mwingine Hayati Dkt. John Magufuli, tumuombee huko alipo.

 

“Niwatake wote walio kwenye chanzo cha maji na maeneo ya maji yanapotoka mlinde miundombinu hii ya maji, serikali tumeleta tu mradi lakini matunzo ya mradi ni nyinyi wenyewe. Mradi huu ni wenu mkiutunza mtafaidika.

 

“Maji ni maendeleo, baada ya kupata maji Longido, Maendeleo mtayaona namna yatakavyofumka hapa. Mtajionea hapa viwanda, maghorofa, lakini pia maji ni uhai na mifugo yetu haitakufa.

 

“Kuna hali ya kutochukuliana hatua, kuna vitendo vya wizi, kuna watu kutokuwajibika kazini, kuna vitendo vya uzembe, upotevu wa mapato, bado mnaoneana shida kuchukuliana hatua, halmashauri piganeni na vitendo hivi, madiwani simamieni maendeleo, wajibikeni vizuri.

 

“Kwa hivi sasa Namanga bado haijakidhi kuwa mji mdogo, vyanzo vya mapato bado vichache, uchumi wake bado upo haujakua vizuri. Tukiitoa Namanga na kuifanya kuwa mji mdogo ni wazi tutaiua Longido. Serikali hii kama ilivyokuwa serikali ya awamu ya tano, ni serikali ya kuwatumikia wananchi, tupeni ushirikiano,” amesema Rais Samia.

 

Leave a Comment