Waandishi Wetu, Dar es Salaam
DIRISHA dogo la usajili lilifungwa rasmi jana na Yanga SC ikaamua kufunga kwa kunasa saini ya straika wa Mwadui FC, Paul Nonga kwa mkataba wa miaka miwili.
Wakati Yanga ikiwa jijini Tanga, sekretarieti ya timu hiyo ilifanya juhudi binafsi kulimaliza suala hilo jijini Dar es Salaam kwenye makao makuu yake Mtaa wa Jangwani, Kariakoo.
Maongezi na mchakato wa zoezi hilo lilianza rasmi jana asubuhi baada ya straika huyo wa zamani wa Mbeya City kutua jijini Dar kwa ndege akitokea Shinyanga kwa ajili ya kukamilisha dili hilo.
Baada ya kukamilika kila kitu baadhi ya viongozi wa Mwadui iliyo chini ya kocha Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ waliwasili jijini kwa ndege majira ya jioni kwa ajili ya kuzima tetesi na kumkabidhisha kijana kwa Wanajangwani hao.
Championi Jumatano lilizungumza na Nonga ambaye alikiri kumalizana na Yanga kila kitu isipokuwa kilichokuwa kimebaki ni yeye tu kutia saini kwa kuwa kuna baadhi ya mambo walikuwa wakisubiri kisha amalize mchezo.
“Tumekubaliana miaka miwili jioni hiihii, kuna kitu nasubiri kikamilike katika levo ya uongozi kisha nitasaini, haliwezi kuingia giza kabla ya sijasaini maana hakuna pingamizi, kila kitu tushamalizana,” alisema Nonga.
Hata hivyo, mpaka gazeti hili linakwenda mitamboni Nonga alikuwa bado kwenye makao makuu ya klabu hiyo, taarifa za ndani zikieleza kuwa lilikuwa likisubiriwa zoezi la kuhamisha fedha za ada ya usajili kwa njia ya elektroniki kutoka kwenye akaunti moja kwenda nyingine.
Kabla ya Yanga, kumwania Nonga awali ilikuwa ikielezwa kuwa inamnyatia mshambuliaji wa Stand United, Elias Maguri lakini ikashindikana na sasa imemalizana na Nonga ikiwa katika kuongeza vifaa kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayoanza kuunguruma hivi karibuni.
Wakati huohuo, upande wa pili wa mahasimu wakubwa wa Yanga, Simba SC nako kunafuka moshi baada ya kiungo wake Mzimbabwe, Justice Majabvi kutakiwa kuvunja mkataba klabuni hapo kama ameshindwa kutelekeza baadhi ya maagizo ya timu hiyo.
Ilikuwa hivi, Majabvi anashinikiza kutafutiwa nyumba mpya ya kuishi yenye hadhi yake katikati ya Jiji la Dar lakini uongozi umegoma kufanya hivyo na kumpelekea Majabvi kutoa masharti kuwa kama vipi bora atolewe kwa mkopo au auzwe.
Hayo yote Simba wameyakataa, wakasisitiza kuwa Majabvi hatolewi kwa mkopo na wala hauzwi na kama ataona ni kero kuendelea kuwepo Simba ni bora avunje mkataba wake, asepe.
“Kulikuwa na kikao leo jioni (jana Jumanne), Majabvi ameshikilia msimamo wake wa kutafutiwa nyumba mpya lakini uongozi umegoma, akatoa masharti na uongozi ukayapinga, wakamwambia kama vipi bora avunje mkataba, aondoke Simba kwa amani, ila naye amegoma kuvunja mkataba na amegoma pia kwenda Mwanza kwa ajili ya mechi ya Toto,” kilisema chanzo makini kutoka Simba.