
IKIWA ni takribani wiki moja tangu kuuawa kwake, maiti ya mwanariadha maarufu nchini Kenya, Agnes Tirop imefanyiwa upasuaji katika chumba cha kuhifadhia maiti ha hospitali ya Iten (ICRH) juzi Jumanne, Oktoba 19 na kufichua mengi kuhusu kilichomuua.
Mwanariadha Tirop ambaye anadaiwa kuuawa kwa kuchomwa kisu na mumewe, uchunguzi huo umebaini kuwa Tirop aliaga dunia kutokana na majeraha ya kudungwa shingoni na vile vile kupigwa na kifaa butu kichwani.
Zoezi hilo lililochukua muda wa saa tatu liliendeshwa na wanapatholojia wawili, mtaalam wa upasuaji wa maiti wa ICRH na mwanapatholijia wa familia.
Akizungumza na waandishi wa habari, daktari Dorothy Njeru alisema tayari wameandaa ripoti na kuwakabidhi maafisa wa upelelezi wa Jinai (DCI). Hata hivyo, Njeru alidinda kufichua ni idadi ngapi ya visu ambavyo marehmu alidungwa akidokeza kwamba ripoti zaidi itatolewa na maafisa hao.
“Kwa jumla, uchunguzi umeonyesha majeraha ya kupigwa kwa kifaa butu,” Njeru alisema. Baada ya kufanyiwa upasuaji, mwili wa mwanaridaha huyo ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Eldoret kusubiri mazishi katika kijiji cha Kapnyamisa, Kaunti ya Nandi.
“Mazishi ya dadangu yataandaliwa Jumamosi. Tunapeleka mwili Eldoret tunapoendelea na mipango ya mzishi,” Limo ambaye ni kakake mkubwa nyota huyo alisema. Mshukiwa mkuu wa mauaji ya mwanariadha huyo Emmanuel Ibrahim Rotich mnamo Jumatayu, Oktoba 18 alifikishwa katika mahakama ya Iten.
Hakimu Mwandamizi, Charles Kutwa aliagiza Rotich azuiliwe katika Kituo cha Polisi cha Eldoret kwa siku 20 kusubiri uchunguzi. Mwanariadha huyo nyota, alikuwa ameanza kupata umaarufu baad ya kuvunja rekodi ya dunia mwezi uliopita aliposhinda mbio za kilometa 10. Alitumia muda wa dakika 30:01 katika mbio za Adizero Road to Records huko Herzogenaurach, Ujerumani.