
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kutoa hukumu kutokana na kutokamilika uandaaji wa hukumu na kuomba kuahirishwa kwa shauri hilo hadi Oktoba 28, 2021.
Hukumu hiyo imeshindwa kutolewa katika kesi inayomkabili Rais wa zamani wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na mwenzake Godfrey Nyange “Kaburu”. Hukumu hiyo ilitarajiwa kutolewa leo Alhamisi, Oktoba 21, 2021 na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
Miongoni mwa Mashtaka yanayowakabili washtakiwa ni pamoja na yakula njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi na kutoa maelezo ya uongo.

Katika shitaka la kughushi linawakabili washitakiwa wote, wanadaiwa walighushi hati ya malipo ya kibiashara ya Mei 28, 2016 wakionyesha kwamba nyasi bandia zilizonunuliwa na Simba zinathamani ya dola 40,577 sawa na zaidi ya Sh milioni 90 huku wakijua kwamba sio kweli.
Pia, katika mashitaka mengine inadaiwa Aveva na Nyange kati ya Machi 10 na Septemba 30 mwaka 2016 waliwasilisha nyaraka za uongo kuonyesha Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za Kimarekani 40,577.