×

Kingai Aeleza Mbowe na Makomando Walivyopanga Kumdhuru Sabaya

KESI ya Uhujumu Uchumi yenye Tuhuma za Ugaidi ndani yake inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
CHADEMA, Mbowe Freeman imendelea leo Jumanne, Oktoba 26, 2021 katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ambapo itasikilizwa na Jaji Mpya.

 

Akisoma maelezo ya mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, Adam Kasekwa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Ramadhani Kingai amesema mtuhumiwa huyo alisema Freeman Mbowe alipanga kumdhuru aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na kwamba Mbowe alisema Sabaya anahatarisha nafasi yake ya kuendelea kuwa mbunge wa Hai.

 

ACP Kingai amesema Mbowe Freeman na wenzake walipanga kumdhuru Sabaya na kulipia vituo vya mafuta katika miji ya Moshi, Mbeya, Mwanza na Dar es Salaam ambapo pia walipanga kufanya vurugu kwenye maeneo yenye mikusanyiko ya watu.

 

Kingai ameiambia Mahakama Kuu kuwa Mbowe alikamatwa takribani mwaka mmoja baada ya kukamatwa kwa watuhumiwa wengine na kuchelewa huko kulitokana na kufanyika kwa upelelezi ili kijiridhisha kuhusika kwake katika njama hizo.

 

ACP Kingai ameiambia Mahakama kuwa Mtuhumiwa Adam Kasekwa alikiri kukutwa na Bastola yenye risasi tatu  pamoja na Dawa za Kulevya aina ya Heroin kete 58 na alikamatiwa wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro.

Hii ni sehemu ya maelezo ya mshtakiwa Adamu kama yalivyosomwa na RPC Kingai: “Mbowe alituelekeza tufuatilie nyendo zake na tumdhuru kwa spray ya sumu. Ling’wenya alifuatilia mtu wa kupata sumu. Tarehe 27 tulirudi Dar na magari mawili pamoja na Mbowe na mlinzi wake.

 

“Baada ya kufika Dar tulifikishwa Mikocheni mimi na Ling’wenya tulipewa Sh 200,000 tujiandae. Baadaye tulipewa nauli turudi Moshi. Agosti Mosi saa 11 alfajiri Mbowe alituita akasema tutekeleze maelekezo ya kumdhuru Sabaya.

 

“Akituonesha picha ya Sabaya na maeneo anauyopenda kutembelea. Alituelekeza baada ya kazi ya Sabaya turudi Dar kutekeleza kazi nyingine nyeti kulipua vituo vya mafuta na kushinikiza maandamano ili Serikaki ionekane imeshindwa maana inatuchukia sisi wapinzani.

 

“Yeye aliondoka kurudi Dar sisi tukabaki kutekeleza kumdhuru Sabaya Tarehe 3 Agosti tulienda eneo la Rao Madukani kwa dada yake Ling’wenya ili kubana matumizi maana Mheshimiwa alituachia Sh150,000

 

“Tulikamatwa na askari tukituhumiwa kukutwa na dawa za kulevya na kupanga njama za ugaidi. Tuhuma hizo ni za kweli na pia kukutwa na silaha ni za kweli na nilikutwa na simu yangu ya Itel.

 

“Nilisaini hati ya kuchukuliwa mali na askari nao wakasaini. Nikachukuliwa kwenda Central Moshi. Uthibitisho haya maelezo ni ya kweli kwa saini.

 

ACP Kingai, muda wa kumaliza kuandika maelezo hayo ilkiuwa ni saa 3, Wakili wa Serikali Mwandamizi SSA Kidando anamtaka ACP Kingai aelezee alichoelezwa na Adamu.

 

“ACP Kingai: Alikiri kukutana na wenzake kwa ajili kwenda kwa Mbowe, alikiri kupewa nauli kwenda Moshi kukutana na Mbowe, alikiri kuwepo Moshi tarehe 24 -26 Julai 2020, alikiri kuwepo yeye na wenzake wawili akiwemo Ling’wenya na mtu mwingine.

 

ACP Kingai: Alikiri tarehe 25 usiku kufanya mkutano yeye na Ling’wenya, Moses Lujenje maarufu Kakobe, Hassan Bwire na Freeman Mbowe.

SSA Kidando, nini kiliendelea? ACP Kingai: Alikiri kwenye mkutano alielekezwa na Mbowe kumdhuru DC Sabaya kwa njia yoyote ile.

 

SSA Kidando. Kitu gani kingine alikueleza? Shahidi pia alikiri kupewa pesa na Mbowe Sh150,000 kukidhi mahitaji hapo Moshi, alikiri Agosti Mosi 2020 alfajiri Mbowe aliwaita tena na kuwapa maelekezo, kwamba wahakikishe wanayafanyia kazi.

 

“Kumdhuru Sabaya na ili wawe na uhakika Mbowe aliwaonyesha picha ya Sabaya kupitia simu yake, aliwalekeza wamalize kazi hiyo ya Moshi halafu warudi Dar kufanya kazi nyingine nyeti.

 

“Alitaja kazi hiyo kwamba walipanga wakalipue vituo vya mafuta, lakini pia kufanya vurugu kwenye masoko na maeno ya watu wengi”.

 

Tofauti na siku nyingine hii leo idadi ndogo ya Wanachama wa CHADEMA wameruhusiwa kuingia ndani ya viunga vya Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kwa ajili ya kufuatilia kesi inayomkabili  Mbowe.

 

Leave a Comment