×

Umoja Wa Ulaya ‘EU’, ZIFF Kuonesha Filamu Mikoa Minne

UMOJA wa Ulaya (EU), Nchini umezindua rasmi uoneshaji wa filamu mbalimbali ikiwemo zile zilizotwaa tuzo mwaka huu wakati wa tamasha la kimataifa la filamu za Nchi za Majahazi Zanzibar (ZIFF) ambapo zitaoneshwa kwenye vituo mbalimbali katika mikoa Minne ikiwemo ya Dar es Salaam, Pwani, Mwanza na Dodoma.

 

Filamu hizo zinatarajiwa kuoneshwa kuanzia siku ya Alhamisi 28 Oktoba mwaka huu  kuanzia saa moja jioni kwenye kituo cha Utamaduni cha Ufaransa (Dar –Alliance Francaise) ambapo filamu ya ‘Binti’ ikitarajiwa kuzindua pazia hilo ikifuatiwa na filamu ya ‘Cocktail’ ya kutoka Ubeligiji.

 

Awali wakizungumza baadhi ya Mabalozi wa nchi za EU, akiwemo Balozi wa Umoja huo, nchini Mhe. Balozi Manfredo Fanti alisema tukio hilo ni la kukuza mashirikiano kwenye sekta ya filamu ikiwemo kupanua wigo wa mashirikiano kiutamaduni wa nchi za Ulaya na Tanzania.

 

Balozi Manfredo Fanti alisema kuwa, wamekuwa kwenye mashirikiano na Tanzania kwa zaidi ya miaka 50 kwa sasa na wataendeleza ushirikiano huo katika kukuza tasnia ya filamu ikiwemo kutoa mafunzo na uwezeshaji mbalimbali kwa wadau wa tasnia ya filamu.

 

Na kuongeza kuwa: ZIFF ni kiungo muhimu kati ya tamaduni za dunia kupitia uoneshaji wa filamu.

“Filamu ni sehemu muhimu ya kuwasiliana kimataifa, kuelimisha jamii na ajira, hasa kwa vijana. Tunashirikiana na ZIFF kupanua wigo wa taaluma ya filamu hapa nchini kupitia mafunzo na maonesho kama haya”. aliongezea.

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa ZIFF, Prof. Martin Mhando aliwashukuru EU na Mabalozi wa Umoja huo kwa kuendelea mashirikiano ya kusaidia filamu nchini ikiwemo kuwezesha mafunzo kwa Wanawake waongoza filamu na pia kusaidia Uandishi wa miswada ya filamu nchini.

 

“Mwaka huu kwenye tamasha la ZIFF tulilenga kuwainua Wanawake kwenye dhamira ya kumuinua Mwanamke katika uwezo wa kuonesha filamu.

 

Hii ni katika kujifunza na kutengeneza filamu zenye maudhui ya mwamke kwani mara kwa mara tumezoea kuona filamu zilizotengenezwa na Wanaume ambazo zina maudhui ya Mwanaume, hivyo ZIFF tukaona tuwape nafasi Wanawake katika kuonesha wanazungumzia mwanamke ndo maana tukaonesha filamu ya Binti iliyoongozwa na Mwanamke” alisema Prof. Mhando.

 

Aliongeza kuwa, filamu nyingi zilizooneshwa mwaka huu kwenye tamasha hilo zilikuwa zikihusu Mwanamke na kuongozwa na Mwanamke sambamba na mafunzo namna ya kuigiza kwenye filamu pamoja na namna ya kuwa mbele ya ‘camera’.

 

Aidha, alisema kuwa, EU wametoa mchango mkubwa kwa kufanikisha kuleta filamu hizo Tanzania Bara ambapo awali walikuwa wakionesha filamu zilizoshinda pekee katika kituo cha Goethe Institute cha Ujerumani.

“ZIFF kila mwaka tulikuwa tukionesha filamu zilizoshinda Goethe Institute, lakini mwaka huu tumeona filamu zile zipelekwe kuoneshwa kwenye vituo vingine hapa nchini hivyo kwa udhamini wa EU tumeweza kusogeza kwenye vituo vya:

 

Dar- Alliance Francaise  kwa kufungua filmu ya ‘Binti’  kutoka Tanzania  na pia kutakuwa na filamu ya Cocktail [Ubeligiji]” na kwa 29 Oktoba  katika kituo hicho hicho cha Dar –Alliance Francaise kutakuwa na filamu ya Sweat, Horn  za kutoka nchi ya Poland na filamu ya Mbuland [Tanzania]”. Alisema  Prof. Mhando.

 

Aidha, kwa filamu hizo pia kwa 5 Novemba mwaka huu zitaoneshwa katika kituo cha Chuo cha St. Augustine [SAUT], Jijini Mwanza kwa kuoneshwa filamu za ‘Underline’ ya kutoka Ujerumani na filamu ya ‘Al Sit’ ya kutoka Sudan 6 Novemba wataonesha filamu zingine kwenye kituo hicho ni ‘Tambien La Iluvia’ kutoka Hispania na filamu ya ‘Al Sit’ ya Sudan.

 

Kwa 12 Novemba mwaka huu, filamu zitaoneshwa katika kituo cha Chuo Kikuu cha Mlimani UDSM kwa filamu za ‘Aurora’ kutoka Finland, Mozizi na Mbuland zote za kutoka Tanzania.

 

Aidha, Prof. Mhando alisema kuwa, tarehe 19 na 20 Novemba mwaka huu katika kituo cha TaSUBa wataonesha filamu za ‘Teghadez Agadez’ kutoka Ubeligiji na ‘If Objects Could Talk’ kutoka Kenya na ‘Joy’s Garden nayo kutoka Kenya ambazo zitaoneshwa 19 Novemba huku tarehe 20 Novemba wakitarajia kuonesha filamu za ‘La Gente Resta’ ya kutoka Italy na ‘Maangamizi (Tanzania ).

 

Kituo kingine ni Chuo Kikuu cha UDOM Mkoani Dodoma tarehe 26 Novemba kwa kuonesha filamu za ‘Martha and Niki’ filamu ya kutoka Sweden na ‘Breaking Ground’ ya kutoka Rwanda.

Aidha, maonesho hayo ya filamu yanatarajiwa kufikia tamati tarehe 27 Novemba mwaka huu katika kituo cha Dar -Alliance Francaise kwa kuoneshwa filamu za ‘Our Lady Of The Nile’ filamu kutoka Ufaransa na Rwanda pia filamu ya ‘Mbuland’ (Tanzania) na filamu ya ‘Letter to My Child from Rape’ filamu ya kutoka DRC.

Prof. Mhando aliomba wadau wa filamu kujitokeza kwa wingi kushuhudia kwenye vituo hivyo bure kabisa.

“Kwa kuonesha filamu zilizoshinda katika tamasha la ZIFF tutaweza kuwaonesha watengenezaji wa  filamu wa Tanzania filamu zenye viwango vya kimataifa na kwa njia hiyo kuwawezesha kujipima wenyewe”. Alimalizia Prof. Martin Mhando.

Na Andrew Chale, Dar.

Leave a Comment