
IMEFAHAMIKA kuwa Kocha Mkuu wa Yanga Mtunisia, Nasreddine Nabi na kiungo wake mkongwe Mrundi, Said
Ntibanzonkiza ‘Saido’ tofauti zao zimekwisha na juzi alikuwepo sehemu ya kikosi kilichocheza dhidi ya
JKT Tanzania.
Yanga ilivaana dhidi ya JKT katika mchezo wa kirafiki uliochezwa kwenye Uwanja wa Avic Town, Kigamboni
jijini Dar es Salaam uliomalizika kwa timu hiyo kushinda bao 1-0 lililofungwa na Yusuph Athumani.
Katika mchezo huo, Saido ndiye alikuwa mpishi wa bao hilo akimpigia pasi nzuri ya kufunga Athumani.
Mmoja wa marafiki wa karibu wa Saido, ameliambia Championi Jumatano kuwa Saido na kocha wake Nabi
wamefikia makubaliano mazuri baada ya hivi karibuni kutofautiana.

Rafiki huyo alisema kuwa katika kuthibitisha hilo, kocha huyo alimuanzisha katika kikosi chake kilichocheza mchezo wa kirafiki dhidi ya JKT.
Aliongeza kuwa upo uwezekano mkubwa wa kuwepo sehemu ya kikosi cha kwanza katika michezo
ijayo ya Ligi Kuu Bara baada ya kumshawishi mazoezini na katika mchezo huo wa kirafiki ambao Saido
alitengeneza bao hilo.
“Ni kweli kabisa hakukuwa na maelewano mazuri kati ya kocha na Saido katika siku za hivi
karibuni na hiyo ilisababisha kuwekwa jukwaani katika michezo mitatu ya ligi na
Ngao ya Jamii.
“Tofauti zao zimemalizika na hivi sasa wapo pamoja sambamba na kuanza mazoezi ya pamoja na wachezaji wenzake.
“Katika kuthibitisha hilo, Nabi alimuanzisha Saido katika kikosi cha kwanza kilichocheza mchezo wa kirafiki dhidi ya JKT, hivi sasa anapambana kumshawishi kocha ili amuingize katika kikosi chake,” alisema rafiki huyo.
Mkurugenzi wa Mashindano wa Yanga Thabity Kandoro aliliambia Championi Jumatano kuwa:
“Kazi imeanza upya na timu inaendelea vizuri, Saido ni mchezaji wa daraja la juu sana na hata mwalimu Nabi
amekubali uwezo wake, shida ni majeraha tu ila kwa sasa amerudi.”
Waandishi: Wilbert Molandi, Careen Oscar na Issa Liponda