Mchekeshaji maarufu kutoka nchini Kenya, Erick Omondi amekamatwa na jeshi la Polisi Nchini humo na kupelekwa katika kituo kikuu cha jeshi hilo mjini Nairobi kufuatia maandamano aliyoyafanya mbele ya Bunge la Kenya.
Omondi ametiwa mbaroni akiwa mita chache kutoka eneo la Bunge la nchi hiyo wakati akijaribu kuandamana kwa madai ya kupambania haki za wasanii wa muziki nchini Kenya kwa kile ambacho amekuwa akikizungumzia mara kadhaa kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, kuhusu kuzorota kwa maendeleo ya Sanaa ya Muziki na wasanii nchini humo, ukilinganisha na wasanii wa Mataifa mengine ya Afrika.
Siku ya juzi Novemba 15, 2021, Omondi alikaririwa akitoa maneno ya kuhamasisha jambo hilo kabla ya kuanza maandamano hayo mapema jana Novemba 16.

“Kesho tunaenda Bungeni kupigania muziki kwa sababu huko ndio kuna Spika!!!. Lakini hekima yangu itaniua siku moja” alisema Omondi.
Katika Video inayosambaa mitandaoni Eric ameonekana akiandamana mita chache mbele ya Bunge la nchi hiyo, hata hivyo maandamano hayo hayakwenda mbali kabla ya kuvamiwa na polisi na kumkamata.
Licha ya kuandamana kwa dhamira ya kupigania haki za wasanii wa muziki wa Kenya, mpaka sasa hakuna msanii yeyote wa muziki kutoka nchini humo, aliyejitokeza kusisimama naye isipokuwa rapa KRG the Don ambaye ameapa kuwa atakwenda kumuona Erick Omondi katika Kituo cha Polisi.
“Eric Omondi amekamatwa mjini akipigania wanamuziki, sijaona, yaani hakuna mwanamuziki aliyesimama naye…. niko njiani naelekea mjini kuhakikisha Erik Omondi anaachiliwa ndani ya Saa mbili,” alisema KRG.