×

Teknolojia ya Wahitimu wa Chuo cha VETA Pwani Yashangaza Wageni Waalikwa

 

DUNIA ikiwa inaelekea kwenye mapinduzi ya kiteknolojia wahitimu wa Chuo cha VETA mkoani Pwani wamewashangaza wageni waliofika kwenye mahafali ya tisa ya chuo hicho kwa kuonesha ufundi stadi mahiri kama wataaluma waliobobea na si wanafunzi waliokuwa wakihitimu jana.

Katika mahafali hayo ambayo mgeni rasmi alikuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Pwani Mussa Ndomba alielezea kushangazwa kwake na uwezo wa hali ya juu aliojionea alipokuwa akitembelea karakana na maabara walizokuwa wakizitumia wahitimu hao.

Akizungumza kwenye mahafali hayo Kaimu Mkuu wa hicho, Madam Clara Kibodya amesema hayo yalikuwa ni mahafali ya tisa ya chuo hicho ambapo wahitimu 207 katika fani tisa walikuwa wakihitimu mafunzo yao.

Madam Clara amezitaja baadhi ya fani hizo kuwa ni pamoja na ufundi magari, umeme wa viwandani, umeme wa majumbani, umeme wa magari, useremala, ushonaji, kutengeneza friji na air condition, usekretari, maabara ya kemia na nyinginezo.

Ameendelea kusema Madam Clara kuwa wahitimu hao walichukua mafunzo hayo kwa kipindi cha miaka miwili na wengine miwili na nusu ambapo pamoja na mafunzo ya chuoni hapo wamekwenda kufanya mafunzo kwa vitendo viwandani na hivyo kuwafanya kuwa wahitimu hao kupata uzoefu kivitendo kama waajiriwa.

Kupitia mafunzo hayo Madam Clara ameiomba serikali na mkoa wa Pwani kwa ujumla kuwapa upendeleo wa ajira wahitimu hao ambao sasa ni mafundi stadi mahiri na si wanafunzi tena.

Pamoja na ajira hizo, Madam Clara amewashauri wahitimu hao wengine kuangalia namna ya kujiajiri wenyewe kutokana na ufundi stadi mahiri walioupata na kujiingizia kipato.

“Niiombe serikali na wadau wengine kwenye sekta za ajira kuwaamini wahitimu wetu hawa ambao kufikia hapa walipo wamepikwa vizuri na kupikika hivyo wawatumie bila shaka kwenye nafasi mbalimbali walizohitimu,” alimaliza kusema Madam Clara.

Naye mgeni rasmi katika mahafali hayo, ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Mussa Ndomba alianza na kushukuru kwa heshima aliyopewa ya kuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo.

Baada ya hapo Ndomba ambaye yeye na msafara wake walizunguushwa kwenye karakana na maabara za chuo hicho na kuoneshwa wanafunzi hao jinsi wanavyojifunza katika fani mbalimbali alipata nafasi ya kuzungumza na wahitimu hao maeneo yao ya mafunzo.

Wahitimu hao walimjibu maswali mbalimbali aliyokuwa akiwauliza kwa jinsi alivyojinea mitambo na mashine mbalimbali za teknolojia ya kisasa wanazojifunzia.

Akizungumza na wanahabari Mwenyekiti huyo alisema;

“Nimezunguuka kwenye karakana na maabara za wahitimu hawa na kujionea mambo mbalimbali na hata nilipojaribu kuwauliza maswali kiukweli walijieleza kiufasaha na kwa kujiamini hali iliyothibitisha kupikwa na kupikika kwao.

“Sisi kama serikali tunahitaji vijana kama hawa na nna imani hata wakienda mtaani watakwenda kufanya kazi zao vizuri sana na kujiingizia kipato.

“Kama Halmashauri ya Mji wa Kibaha kupitia fungu letu na alisilimia kumi ya mapato ya ndani ambalo huwaga tunalitenga kinamama asilimia 4, vijana asilimia 4 na walemavu asilimia 2 tunaona kabisa kuwa vijana hawa ndiyo wanaostahili hizo fedha kwa ajili ya kujiendeleza.

Pamoja na hayo sisi kama Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Serikali na taasisi nyingine huu sasa ndiyo wakati muafaka wa kuondoa hofu na kuwapa tenda mbalimbali wahitimu wanaotoka chuo hiki kwa kazi mbalimbali kama vile za ujenzi, umeme, utengenezaji fenicha, ushonaji wa sare, suti na mavazi mengine yanayoweza kuhitajika.

Nichukue nafasi hata kuwaambia Tanroad nao kuwatumia wahitimu wa chuo hiki katika kazi zao mbalimbali na kuacha dhana iliyopitwa na wakati ya kusema kumuajiri mtu mpaka awe na uzoefu kazini wa miaka kadhaa hawa tayari wameshaiva,” alimaliza kusema mwenyekiti huyo.

Leave a Comment