
Rais Samia Suluhu Hassan amewaomba wakazi wa Mbagala kuwa watulivu wakati akitatua changamoto zao kwa kile alichokibainisha kuwa amerithi kasi ya ufanyaji kazi.
Pia ameahidi kuifanya Mbagala kuwa wilaya mara tu uchumi wa nchi utakapotengamaa baada ya ugonjwa wa virusi vya korona (Uviko-19) kupungua.
Samia ameyasema hayo leo Ijumaa Desemba 3, 2021 wakati akisalimiana na wakazi wa Mbagala akiwa njiani kuelekea Mkuranga mkoani Pwani.
Akizungumza na wakazi hao amesema changamoto zao ni changamoto za Serikali, na wanazifahamu akiahidi kuwa anakwenda mbio nyingi kutafuta fedha.
“Ndugu zangu tupeni muda, nina miezi nane sasa lakini mmeona spidi yangu ninavyokwenda, nimerithi spidi na ninakwenda spidi, nitakwenda kufanya kazi kadri ninavyoweza kuondosha hizi changamoto,” amesema Samia.
Amesema anajua changamoto kubwa ya ya machinga iliyopo sasa kwa sababu yeye ndiyo aliyopanga na amewataka kukubali kile kinachofanyika huku akisema maeneo waliyopelekwa yatakuwa bora sana.
“Tunahangaika kutafuta fedha kuwajengea miundombinu mizuri ili mkae pale mfanye kazi zenu, kwa wale ambao hakuna safari za mabasi tunajitahidi kuwaambia Latra watengeneze ili daladala zipite huko wateja wapatikane,”
“Ndugu zangu itazameni Mbagala leo inavyopendeza na awali vibanda vilipokuwa vimejaa barabarani, tunawahakikishia kuwa huko mliko watu watakuja na miundombinu itakuja kwa sababu nia yetu ni tujenge masoko ya machinga yatakayofanya kazi saa 24, tuweke vyoo, umeme, maji na kila kitu,”
Amesema ili kuhakikisha hilo wanahangaika kutafuta fedha huku na kule hata ikibidi za mkopo kama ilivyokuwa za madarasa ili kazi ifanyike kwa kushirikiana na Halmashauri.
Amesema wanaandaa mradi mkubwa wa halmashauri kuweza kukopeshwa moja kwa moja kwa ajili ya kazi hiyo na kazi nyingine ikiwemo za barabara.
Kuhusu kuifanya Mbagala kuwa wilaya, Samia amesema nchi ipo katika changamoto ya uchumi kutokanana ugonjwa wa Uviko 19 hivyo ni ngumu kuanzisha maeneo mapya ya utawala.
“Mbagala kuwa wilaya hata mimi naliunga mkono kwa sababu nikipita hapa ninavyoona watu wa Mbagala nasema hii inafaa kuwa wilaya peke yake lakini kwa sasa hivi nimeshindwa kufanya hivyo kutokana na hali ya uchumi lakini ikitengamaa naahidi wilaya ya kwanza kukatwa kuwa wilaya ndani ya Tanzania itakuwa Mbagala,”
Kuhusu hospitali ya Mbagala Zakhemu kukabiliwa na changamoto aamesema wanashindwa kuipanua kwa sababu eneo ni dogo licha ya kuitengeneza na kuiongezea uwezo lakini pia itajengwa hospitali nyingine ya wilaya.
Awali akitoa salamu zake Mbunge wa mbagala, Abdallah Chaurembo alimuomba Rais Samia kuangalia namna ya kuifanya Mbagala kuwa wilaya kwa sababu imejitosheleza kwa vitu vingi na ina idadi kubwa ya watu.
“Tayari Dawasa, Tanesco, TTA vyote vikiwa na level ya wilaya vipo hapa, tukuombe tu Mheshimiwa Rais tumebakiza tu Mkuu wa Wilaya naamini, nafahamu changamoto za kibajeti lakini Mungu akijaalia mambo yakikaa sawa tuangalie kwenye hili wilaya ya Mbagala itatusaidia sana,” amesema Chaurembo.
Alimuomba pia Rais kutatua changamoto zinazoikabili hospitali ya Mbagala Zakhem ambayo ni ya ngazi ya wilaya na inahudumia watu wengi.