
MORINE Amatusi Liyumba ni binti mrembo wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), marehemu Amatus Liyumba ambaye alifungwa jela Mei 23, 2010 kwa makosa ya kutumia vibaya ofisi ya umma kisha aliachiwa huru Septemba 24, 2011 na kufariki dunia Aprili 15, 2016.
Wakati Liyumba anafariki dunia, binti yake huyo alikuwa mahabusu baada ya kukamatwa kwenye msala wa kusafirisha dawa za kulevya (unga) kule mkoani Lindi.
Hata hivyo,ujio wa habari hii ni kuachiwa huru kwa Morine baada ya kukaa mahabusu kwa miaka 9 na kukutwa hana hatia, lakini nyuma ya pazia kuna mastaa wengi; hasa wa kike na watoto wa mjini ambao wanaendelea kusota jela katika magereza mbalimbali duniani baada ya kukamatwa na dawa za kulevya kwa staili ya Morine.
Kuachiwa kwa Morine kunakuja miezi kadhaa baada ya kuachiwa kwa Jacqueline Fitzpatrick Cliff au Jack Patrick aliyetumikia kifungo cha miaka 8 jela nchini China kufuatia kukamatwa na dawa za kulevya huko Macau, Hong Kong.
Pia ni mwaka mmoja baada ya kuachiwa kwa Binti Kiziwi ambaye naye alifungwa kifungo cha miaka 7 nchini China kwa msala huohuo wa madawa ya kulevya na kwa staili ileile ya kutumwa na mapapa wa biashara hiyo.
TUANZE NA KISA CHA MORINE
Siku chache kabla ya kukamatwa kwa Morine, Gazeti la IJUMAA lilifanya mahojiano naye nyumbani kwa baba yake, Mikocheni B jijini Dar juu ya baba yake huyo kukamatwa na kukabiliwa na kesi mbaya ya ubadhirifu wa mali ya umma na matumizi mabaya ya ofisi ya umma (BoT).
Baba yake alikuwa anatuhumiwa kwa ufisadi katika ujenzi wa majengo pacha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) unayoyaona pale Posta Mpya jijini Dar.
Katika mahojiano hayo, Morine alilieleza gazeti hili kwamba alikuwa binti wa kidato cha nne katika Sekondari ya Mbezi-Beach, Dar lakini ndiye alikuwa msimamizi wa familia hiyo ya kitajiri baada ya baba yake kutupwa jela na mama yake kuwa amefariki dunia.
Morine alikuwa wazi kueleza mambo mengi ya familia yake ambayo kwa busara ya chumba cha habari ilionekana si mambo ya kuyaweka wazi kwa kuwa yalisemwa na binti mdogo, lakini yakiwa ni mambo makubwa juu ya baba yake dhidi ya Serikali ya Tanzania chini ya utawala wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Mrisho Kikwete ‘JK’.
ALITAKA KUWA STAA KULIKO WEMA
Mwishoni mwa mahojiano hao, Morine alieleza dhamira na ndoto yake ya siku moja kuwa staa mkubwa kuliko mwigizaji Wema Sepetu na kuishi maisha ya kifahari, akiomba habari zake ziandikwe na Gazeti la IJUMAA atakapokuwa staa mkubwa.
Hata hivyo, haukupita muda mrefu; Morine, akiwa Maisha Club ya wakati ule jijini Dar, mwaka 2012 alipata mpenzi ambaye ndiye aliyekuja kumsababishia matatizo makubwa, akijikuta mahabusu kwa miaka 9; aliingia akiwa na umri wa miaka 22, sasa ameachiwa huru bila hatia akiwa na umri wa miaka 30.
Simulizi ya kukamatwa kwake inaelezwa Mahakama ya Lindi mapema wiki hii kwamba, Morine alijitetea kuwa, yeye alikutana na mwanaume huyo Maisha Club jijini Dar ambapo jamaa huyo alimkatia tiketi ya ndege na kumtaka wakutane hotelini mkoani Lindi.
Morine anasema alifanya hivyo akiamini jamaa huyo ni mtu safi, lakini alipofika Lindi alijikuta mikononi mwa Polisi wa kudhibiti dawa za kulevya na alishangaa kusikia watu aliokuwa nao walikutwa na kilo 210 za Heroin na Cocaine.
Washtakiwa wengine wawili kwenye kesi hiyo wamehukumiwa vifungo vya miaka 40 jela na faini ya mabilioni.
Hata hivyo, katika kesi hiyo alitajwa mtu ambaye anadaiwa kufungwa nchini Marekani aitwaye Shkuba na wenzake wawili akiwemo mmoja aliyetajwa kwa jina la Tiko.
JACK PATRICK NA BINTI KIZIWI
Jack Patrick na Binti Kiziwi walikuwa ma-video queen na mastaa wakubwa wa mwanzoni mwa miaka ya 2010 waliokuwa wakiishi maisha ambayo mabinti wengi mjini waliwatamani, lakini nao walijikuta mikononi mwa Polisi nchini China kisha kuhukumiwa kifungo cha miaka 8 kwa Jack Patrick na miaka 7 kwa Binti Kiziwi huku baadhi ya Wabongo wakihofia kunyongwa kwao.
Mazingira ya kukamatwa kwao na kujikuta wakisota magerezani yanafanana kwani wote walidaiwa kukamatwa na unga, lakini wao wakiwa kama punda na nyuma yake kukiwa na vigogo waliowatuma.
KISA CHA MASOGANGE
Unakikumbuka kile kisa cha kukamatwa kwa marehemu Masogange nchini Afrika Kusini akiwa na dawa za kulevya? Ndivyo ambavyo mabinti wengi wa Kitanzania wanasota kwenye magereza ya nchi mbalimbali kwa kutumwa kusafirisha unga na mapapa wa biashara hiyo huku wakiahidiwa kuja kuishi maisha ya kifahari.
MDOGO WA WEMA
Kipo kisa kingine cha binti aitwaye Allu Murugwa ambaye ilisemekana ni mtoto wa mjini ambaye ni mdogo wa mwigizaji Wema Sepetu ambaye mwaka huu alikamatwa na wenzake watatu kwa msala wa biashara ya dawa za kuelevya.
Allu alikamatwa nyumbani kwa mpenzi wake maeneo ya Kijitonyama jijini Dar ambapo ilisemekana kwamba mwanaume huyo ndiye aliyemponza.
Allu alikamatwa na watuhumiwa wengine waliotajwa kwa majina ya Joseph Dalidali, Said Mbasha na Fatima Shomari; wote wakazi wa wilayani Kinondoni, Dar ambao hadi sasa wanasota mahabusu wakisubiri hukumu ya kesi yao ya kukutwa na kilo 30.6 za Heroin.
HOFU KANAL TOP KUNYONGWA
Kanal Top alikuwa mwimbaji mkubwa wa muziki wa Dansi akitumikia bendi mbalimbali Bongo hasa Akudo Impact ambaye mwaka 2014 zilizagaa taarifa kuwa haonekani, lakini baadaye zikavuma tetesi kwamba alikamatwa nchini China akisafirisha madawa ya kulevya.
Baadaye, wanamuziki wenzake kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia walianza kuingiwa na hofu baada ya kusikia madai kwamba huwenda amenyongwa, lakini naye kama alikuwa akisafirisha, basi alitumika kama punda tu wa kusafirisha.
KISA CHA MORRIS SEMKWAO
Kisa kingine kinamhusu kijana wa mjini, Morris Sekwao au Junior wa jijini Dar ambaye naye mwaka 2015 alikuwa haonekani kwenye viunga ndipo zikasambaa taarifa kwamba alikamatwa nchini Nigeria akituhumiwa kunaswa na unga.
Ilisemekana kwamba, Junior alipata mkasa huo nchini Nigeria ambapo alikuwa akitokea Bongo na mzigo huo.
Alikamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Murtala Muhammed (MMIA) uliopo Ikeja, Lagos nchini Nigeria, akiwa na unga huo aina ya Ephedrine wenye uzito wa kilo 25.
Aina ya dawa alizokamatwa nazo ni kama ile aliyokamatwa nayo Masogange huku ikisemekana kuwa ‘doni’ aliyembebesha mzigo (aliyemfanya punda) Junior ndiye yuleyule aliyedaiwa kumbebesha Masogange.
SHAMIM NA MUMEWE JELA MAISHA
Wanandoa, Shamim Mwasha mumewe, Abdul Nsembo ni watoto wa mjini waliohukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha unga.
Hukumu hiyo ilitolewa Machi 31, 2021 na Jaji Elinaza Luvanda wa Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi almaarufu Mahakama ya Ufisadi baada ya kuwatia hatiani.
Shamim; mmiliki wa Blog ya 8020 na mumewe Nsembo almaarufu Abdulkadinda, walikuwa wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kusafirisha unga aina ya aina ya Heroin gramu 439.70.
WANANDOA WENGINE
Ukimwacha Shamim na mumewe, Januari 19, 2018, wanandoa wengine kutoka Tanzania, Baraka Malali na mkewe Ashura Musa nao walikamatwa kwa tuhuma za dawa za kulevya kwenye Uwanja wa Ndege wa Baiyun, Guangzhou nchini China.
Wawili hao walikamatwa na pipi 129 za dawa hizo za kulevya aina ya Heroine ambapo hadi sasa kesi yao inaendelea nchini humo na wao wakiendelea kusota nyumba ya nyundo; yote kwa tamaa ya kutaka maisha ya kifahari.
SHKUBA NA WASHIRIKA WAKE
Mwaka 2019 Shkuba; mtoto wa mjini, alikuwa miongoni mwa Watanzania tisa waliohukumiwa kifungo nchini Marekani kwa kujihusisha na usafirishaji wa unga aina ya Heroine.
Mwanasheria wa Marekani, Ryan Patrick, mbali na kumtaja Shkuba, pia aliwataja washirika wake wengine kutoka Tanzania ambao ni Ernest Mbwile, Abdulahtif Maalim, Ibrahim Madega, Tiko Adam, Iddy Mfullu, Mohammed na Daud Vedasto ambao hadi sasa wanasota jela.
Mbali na hao, wapo warembo na vijana wa mjini wengi kwenye magereza ya nchi mbalimbali kama India, China, Pakstan, Italia, Brazil, Nigeria, Ghana na kwingineko.