×

Kipindupindu Chapindukia Nkasi, 37 Walazwa

UGONJWA wa mlipuko wa Kipindupindu umeibuka wilayani Nkasi mkoani Rukwa ambapo wagonjwa 37 wameripotiwa katika kijiji cha Forodhani, Kata ya Korongwe.

 

Akitoa taarifa kwenye Kikao cha Dharura cha Kamati ya Afya ya Msingi, Mganga Mkuu wa wilaya Nkasi, Benjamin Chota amesema kuwa taarifa za kwanza za kuwepo kwa wagonjwa wa kipindupindu zililipotiwa Desemba 2, mwaka huu ambapo wagonjwa watatu walilipotiwa kuwapo katika Zahanati ya Korongwe.

 

Amesema kuwa baada ya taarifa hiyo timu afya ya wilaya kwa kushirikiana na timu ya mkoa walielekeza nguvu katika kijiji hicho na baada ya kuchukua sampuli na kuzipima ilibainika kuwa ni ugonjwa wa kipindupindu ndipo walipoanza kuchukua hatua mara moja za kukabiliana na ugonjwa huo.

 

Amedai kuwa waliweka kambi kwa ajili ya wagonjwa wa kipindupindu na kuwa hadi sasa wagonjwa walioripotiwa na kupata matibabu ni 37 ambapo walioruhusiwa kurudi nyumbani ni 25 na waliopo wodini wakiendelea kupata matibabu ni 12 lakini hadi sasa hakuna kifo kilichoripotiwa kutokana na ugonjwa huo.

 

Mkuu wa wilaya Nkasi, Peter Lijualikali kwa upande wake ameitaka timu ya wataalamu kuhakikisha wanachukua hatua zaidi ili kuona kuwa ugonjwa huo hautoki nje ya kata hiyo na kubwa ni kuona unadhibitiwa palepale uliopoibuka.

 

Amewataka wataalamu wa afya kuhakikisha wanalisimamia suala zima la usafi katika maeneo yote ya wilaya Nkasi kwani Kipindu pindu ni matokeo ya uchafu na kuwa hatamvumilia mtu ambaye kwa uembe wake utapelekea ugonjwa huo kusambaa maeneo mengine.

 

Amedai kuwa sheria za kukabiliana na uchafu zipo kinachotakiwa ni kuzitumia ili kuweza kuona mazingira ya kuishi yanakua safi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha maji ya kunywa yanachemshwa au yanawekwa dawa.

Leave a Comment