
PAMBANO la Ligi Kuu Bara kati ya Kagera Sugar na Simba lililokuwa lipigwe leo Saa 10:00 jioni, kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba limeahirishwa kutokana na nyota 16 wa Wekundu wa Msimbazi kugundulika wanaugua mafua makali na kifua.
Sababu za kuhairishwa kwa mchezo huo kupitia taarifa ya Bodi imesema; “Kitabibu wachezaji 16 wa Simba kati ya 22 waliosafiri kwenda Bukoba, wameonekana kuwa na dalili za mafua na kukohoa hali inayochangiwa na mabadiliko ya hali ya hewa (Seasonal Infulenza) kama ilivyotokea katika miaka ya nyuma.
Taarifa hiyo imeeleza zaidi ikisema kwa mazingatio ya kanuni ya 34:1 (1.3) ya Ligi Kuu, mchezo huo umehairishwa na utapangiwa terehe nyingine kwa mujibu wa kanuni ya 34:2 ya Ligi Kuu.
Kanuni ya 34:1 (1.3) inaeleza mchezo unaweza kuhairishwa kutokana na sababu yoyote kati ya sababu ya dharua/yenye msingi itakavyokubaliwa na TFF.
Kanuni ya 34:2 inaeleza mchezo wowote uliohairishwa chini ya kanuni 34(1.1-1.3) utapangwa tena katika tarehe itakayoamuliwa na TPLB isipokuwa kama utaahirishwa chini ya kanuni 34(1.4) utachezwa siku inayofuata au muda mwingine wa karibu zaidi kadiri ratiba inavyoruhusu.