Naibu Waziri Ofisi ya Rais tawala za Mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) anayeshghulikia Afya, Dkt. Festo Dugange ameagiza kufanyika kwa uchunguzi wa matumizi ya fedha za ujenzi wa wodi tatu katika hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi Vijijini.
Dkt. Dugange ametoa maagizo hayo baada ya kukagua ujenzi huo ambao ni wodi ya watoto, wanawake na wanaume, ambapo alibaini kiasi kikubwa cha fedha kimetumika na fedha zilizobaki ni kidogo lakini ujenzi haujakamilika.
Amesema halmashauri hiyo ilitakiwa kupokea kiasi cha sh. Milioni 500 ili kukamilisha ujenzi huo na badala yake ilipokea Tsh. Milioni 482, lakini matumizi ya fedha yamekuwa makubwa kuliko ujenzi wenyewe.

“Mpaka sasa mmesema mmetumia kiasi cha Tsh. Milioni 434, mmebakiza Tsh Milioni 48 kiasi ambaco hakiwezi kukamilisha ujenzi huu, hapa kuna dalili kubwa za wizi wa fedha za umma, mmetumia kiasi kikubwa na ujenzi umefikia asilimia 50,” amesema Dugange.
Kutokana na hali hiyo Naibu Waziri huyo ameagiza vyombo vyote vya kiuchunguzi pamoja na ofisi ya Mkurugenzi, kufanya uchunguzi haraka juu ya matumizi ya fedha katika ujenzi huo na wahusika wote watakaobainika wachukuliwe hatua kali za kisheria.
“Kwa kiasi hiki ambacho kimebaki hakika hakiwezi kukamilisha ujenzi huu, halmashauri tafuteni mbinu za wapi mtapata fedha mkamilishe ujenzi, wale wote ambao wametafuta fedha hizi wabanwe na wazirejeshe na ndizo hizo zikamilishe ujenzi na siyo kutafuta mapato ya ndani,”
Aidha ameagiza ujenzi wa wodi hizo kufikia Januari 30, 2022 uwe umekamilika huku akitaka uchunguzi aliouagiza ukamilike ndani ya siku 30 na taarifa ipelekwe ofisi za Tamisemi Dododoma.