
MWANZONI msanii Rayvanny alikuwa akifanya muziki wa rap kabla ya kuanza kuimba. Mwaka 2011 aliibuka mshindi katika mashindano ya free style pale Coco Beach jijini Dar.
Wakati huo alijulikana kama Raymond, akatafuta tobo la kutoka kimuziki chini ya Lebo ya Tip Top Connection kwa mtu mzima Babu Tale.
Aprili, 2016 ndipo alipoanza kuona mwanga baada ya kusainiwa kwenye Lebo ya WCB ya mtu mzima Diamond Platnumz.
Wimbo wake wa kwanza ndani ya WCB au Wasafi ulikuwa ni Kwetu. Usiku wa Juni 25, 2017 katika Ukumbi wa
Microsoft Theater Centre, Los Angeles nchini Marekani, Rayvanny alipokabidhiwa Tuzo ya BET kupitia Kipengele cha Viewer’s Choice Best New International Act na kuwa msanii wa kwanza na pekee wa Tanzania kushinda tuzo hiyo hadi sasa.

Ikumbukwe Diamond amewania Tuzo za BET zilizoanza kutolewa Juni 19, 2001 mara tatu bila ushindi wowote, alifanya hivyo mwaka 2014, 2016 na 2021, lakini kijana wake anayo kabatini kwake.
Hivyo, Rayvanny akawa msanii wa pili Afrika Mashariki kushinda tuzo hiyo baada ya Eddy Kenzo wa Uganda ambaye aliishinda mwaka 2015 na kuwa msanii wa kwanza kwa ukanda huo.
Ferbruari, 2020 Rayvanny aliachia Extended Playlist (EP) yake ya kwanza, Flowers iliyofanya vizuri hadi kufanikiwa kuingia kwenye hatua ya kujadiliwa (consideration) kwa ajili ya kuingia kuwania Tuzo za Grammy.
Mwaka mmoja baadaye, yaani Februari 1, 2021 Rayvanny aliachia albam yake ya kwanza ya Sound From Africa ikiwa na ngoma 23 alizowashirikisha wasanii 20 wa Tanzania na nchi nyingine za Afrika.
Sound From Africa iliweka rekodi Afrika Mashariki kwa kufikisha wasikilizaji (streams) zaidi ya milioni 100 ndani ya wiki moja pekee tangu ilipotoa.
Rayvanny akiwa chini WCB, Machi 2021aliweza kuanzisha lebo yake ya Next Level Music (NLM) akiwa ni msanii kwanza kufanya hivyo kwani Rich Mavoko na Harmonize walijiengua kwanza WCB ndipo wakaanzisha lebo zao, lakini Rayvanny amefanya hivyo bado akiwa ndani ya Wasafi.
Septemba 24, 2021 alimtoa msanii wa kwanza wa NLM, Mac Voice ambaye tayari alikuwa ameshasikika kwenye Bongo Fleva kwa kipindi cha nyuma ambapo alikuwa chini ya usimamizi wa msanii Chege.
Mac Voice akaachia EP iitwayo My Voice EP yenye ngoma tano ambapo amemshirikisha Rayvanny kwenye ngoma mbili, nayo ilifanya vizuri hadi kufikisha wasikilizaji zaidi ya milioni 10 kwenye mitandao ya iTunes, Spotify,
Audiomack na Boomplay na Play Music kwa kipindi cha mwenzi mmoja tu.
Kufuatia kufanya vizuri, Mac Voice aliteuliwa kuwania Tuzo za African Entertainment Awards USA (AEAUSA) huko Marekani ambapo alitupwa kwenye Kipengele cha Msanii Bora Chipukizi 2021.
Wakati Mac Voice akiendelea kufanya vizuri, Oktoba 29, 2021 Rayvanny aliachia EP yake ya pili ya New Chui yenye ngoma sita huku akimshirikisha msanii mmoja tu ambaye ni Abby Chams.
EP hiyo ilitoka wakati Rayvanny na Maluma wamesharekodi na kufanya video ya wimbo wao, Mama Tetema ambao ndiyo uliwapa nafasi ya kwenda kutumbuiza kwenye jukwaa la MTV Europe Music Awards (MTV EMA) 2021 na kuwa msanii wa kwanza kutoka Afrika kutumbuiza katika tuzo hizo ikiwa ni mwendelezo wa
kufanya mambo makubwa katika muziki wake.
Ukiacha yote hayo, lakini Rayvanny ndiye msanii wa pili Afrika Mashariki ambaye ameongoza kwa kusikilizwa baada ya Diamond Platnumz
STORI; SIFAEL PAUL, DAR