×

Yaliyojiri Mahakamani Kesi ya Sabaya

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Arusha leo Jumatano Desemba 29, 2021 imeshindwa kutoa uamuzi mdogo katika kesi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita baada ya mawakili wa utetezi kushindwa kufika mahakamani.

 

Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 27 ya mwaka huu, mbali na Sabaya watuhumiwa wengine ni Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.

 

Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Patricia Kisinda upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Felix Kwetukia na Mwendesha Mashitaka wa Takukuru, Jacob Piyo.

 

Wakili Kwetukia alieleza mahakama kuwa upande wa watuhumiwa hakuna wakili hata mmoja na watuhumiwa wote wapo mbele ya mahakama hiyo.

 

“Leo upande wa watuhumiwa hakuna wakili hata mmoja ila watuhumiwa wote wapo. Shauri lilikuja kwa ajili ya uamuzi mdogo na kwa kuwa watuhumiwa wana uwakilishi wa mawakili ambao kwa siku ya leo hawapo,”alisema na kuongeza.

 

“Mahakama inakuwa haipo katika nafasi ya kutoa uamuzi huo mdogo labda kama washitakiwa wataondoa uwakilishi. Tunaomba tupangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya kutoa uamuzi huo mdogo,”

 

Hakimu Kisinda aliwauliza watuhumiwa hao iwapo bado wanauwakilishwa na mawakili wao ambapo waliieleza mahakama bado wanawakilishwa.

 

Hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 3, 2022 kwa ajili ya uamuzi huo mdogo ambapo pia aliutaka upande wa Jamhuri kuhakikisha shahidi aliyekuwa anaendelea kutoa ushahidi wake anakuwepo mahakamani hapo kwani baada ya uamuzi huo ataendelea.

 

Watuhumiwa hao wanatetewa na Mawakili Mosses Mahuna, Fauzia Mustafa, Edmund Ngemela, Sylvester Kahunduka na Fridolin Bwemelo.

 

Uamuzi huo mdogo ulipangwa kutolewa baada ya mawakili wa utetezi kuwasilisha pingamizi kutolewa na wakati shahidi wa 13 wa Jamhuri, Ofisa Uchunguzi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru),Ramadhan Juma, akiendelea kutoa ushahidi.

 

Desemba 17 mwaka huu, akiwasilisha hoja ya pingamizi hilo Wakili Mahuna aliieleza mahakama kuwa shahidi huyo hana uwezo wa kutambua watu kupitia ripoti hiyo ambayo hajaiandaa yeye na wala siyo mtaalamu kutoka maabara ha kiuchunguzi.

 

Alisema kuwa shahidi wa nane, Johnson Kisaka (Ofisa uchunguzi kutoka maabara ya kiuchunguzi ya Takukuru), aliieleza mahakama kuwa hawezi kumtambua mtu kupitia ripoti hiyo.

 

Alieleza kuwa iwapo Juma atawatambua watu hao wakati hajashiriki wala kuandaa ripoti hiyo atakuwa anatoa maoni yake hivyo kuomba mahakama isimruhusu kutambua watu kwenye ripoti ambayo hajaandaa yeye.

 

Kwa upande wao mawakili wa Serikali waliomba mahakama hiyo kutupilia mbali pingamizi hilo kwani halina misingi ya kisheria wala mashiko na kuwa shahidi huyo alikuwa anataka kuionyesha mahakama kile alichokuwa ameeleza kukibaini kwenye ripoti hiyo iliyopo kwenye flash.

 

Awali kabla ya pingamizi hilo, Wakili Kwetukia aliiomba mahakama shahidi huyo atambue vielelezo mbalimbali ikiwemo CCTV footage ambayo ilikuwa kwenye ripoti aliyoandaa na kuwasilisha mahakamani hapo kama kielelezo shahidi wa nane (Kisaka).

Leave a Comment