×

Tembo Warriors Waitwa Uturuki

MCHEZAJI wa timu ya taifa ya soka la wenye ulemavu, Tembo Warriors, Frank Ngailo ‘Mbappe’ anatarajiwa kwenda Uturuki kufanya majaribio kwenye klabu ya Izmir BBSK.

 

Ofa ya Ngailo imekuja baada ya kuchaguliwa kuwa mchezaji bora katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (CANAF) kwa wenye ulemavu yaliyofanyika nchini Novemba 25 hadi Desemba 10, mwaka jana.

 

Izmir ni klabu kubwa inayoshiriki Ligi Kuu ya Watu Wenye Ulemavu Uturuki na Ngailo ambaye maarufu hujulikana kama Mbappe, jina lake lilipelekwa kwenye timu hiyo na nahodha wa klabu hiyo, Mahmud Tawfik ambaye ni mchezaji wa timu ya taifa ya Misri baada ya kumuona kwenye mashindano ya Afrika.

 

Akizungumza na gazeti hili jana, Mbappe alisema amepata nafasi hiyo baada ya mchezaji wa timu ya taifa ya Misri ya watu wenye ulemavu, Tawfik kumuona kwenye mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika yaliyofanyika mwaka jana, Dar es Salaam.

 

“Baada ya mashindano Tawfik aliniita na kuniomba namba ya simu na kuniambia kocha wake anataka kuzungumza na mimi, siku ya pili kocha huyo alinipigia simu na kuniuliza kama ningependa kujiunga na klabu yao, nikamwambia subiri nizungumze na uongozi wangu,” alisema Ngailo.

 

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Watu Wenye Ulemavu Tanzania (TAFF), Peter Sarungi alisema ni heshima kubwa kuwa na mchezaji anayekwenda kucheza soka la kulipwa kwani itaongeza chachu kwa wengine.

 

“Ni fahari na heshima kwa TAFF na Tanzania kwa ujumla, pia ni chachu kwa wachezaji wengine kuongeza bidii hasa kipindi hiki tunachojiandaa kucheza Kombe la Dunia,” alisema Sarungi.

 

Mashindano ya Kombe la Dunia kwa wenye ulemavu yatafanyika Uturuki Oktoba mwaka huu na Afrika itawakilishwa na Tanzania, Misri, Liberia na Morocco.

Leave a Comment