
MWAKA 2021 hauwezi kusahaulika kwa baadhi ya wasanii au watu walio kwenye tasnia ya muziki Bongo kwani kuna walionunua magari ya kifahari na wapo walionunulia na mabosi wao kutokana na kile kilichoelezwa kwamba ni utendaji wao murua.
Pamoja na kupita kwenye kipindi kigumu cha janga la UVIKO-19, lakini wamejitahidi au kupambana na kufanikiwa kunoga na ndinga kali;
DIAMOND PLATNUMZ -ROLLS ROYCE CULLINAN
Diamond Platnumz ndiye kinara aliyenunua magari ya bei mbaya zaidi Bongo baada ya kwenda Dubai na kuvuta gari la kifahari mwezi Julai, 2021 na aina yeke ni Rolls Royce Callinan. Gari la aina hii mwaka uliopita walinunua pia wasanii wa Nigeria, Davido na Burna Boy.
Diamond hakuishia hapo kwani alinunua pia magari mawili ya kifahari aina ya Cadillac Escalade na kumfanya kuwa na magari ya kifahari saba hadi sasa. Mbali na magari hayo, Diamond pia anamiliki magari mengine kama Toyota Land Cruiser V8 (yapo mawili) Toyota Prado pamoja na BMW X6; lile la bluu lenye jina la Platnumz balada ya namba ya usajili.
JUX -MERCEDES BENZ
Huyu ni mkali wa RnB Bongo ambaye Julai, 2021 alinunua gari jipya aina ya Mercedes Benz. Mara baada ya kulivuta ndinga hilo, Jux aliamua kulipa jina la Huddah; jina la mrembo wa nchini Kenya ambaye amewahi kuhusishwa naye kimapenzi. Kabla ya hapo, Jux alikuwa anasukuma gari aina ya Toyota Fuga.
NANDY- RANGE ROVER EVOQUE
Nandy ni mrembo na ni msanii wa Bongo Fleva ambaye mwaka 2021 alifanya makubwa yakiwemo matamasha yake ya Nandy Festival yaliyofanyika Tanzania Bara na visiwani Zanzibar.
Baada ya matamasha hayo, Nandy alionesha gari lake jipya aina ya Range Rover Evoque likiwa mbele ya ofisi yake na amelipa jina la white horse; yaani farasi mweupe.
Mbali na ndinga hilo, Nandy anamiliki mandinga mengine kama Land Rover Discovery, BMW X1, Mercedes Benz, Toyota Alphard, Toyota Harrier na Toyota Noah anayoyatumia katika shughuli zake za kila siku.
RAYVANNY –TOYOTA LAND CRUISER PRADO
Pamoja na kwamba, huwa hapendi kujionesha, lakini mwaka 2021 alivunja ukimya na kujinunulia gari aina ya Toyota Land Cruiser Prado baada ya kutajwa kama msanii wa pili anayeongoza kwa mauzo ya muziki wake kwenye mitandao mbalimbali ya kusikiliza, kutazama, kuuza na kununua muziki akiachia albam moja ya Sound From Afrika na EP ya New Chui.
MAUA SAMA –TOYOTA VANGUARD
Miongoni mwa wasanii wa kike waliofanya vizuri yumo Maua Sama. Ametisha na ngoma nyingi, lakini ile ya Zai imempaisha kimataifa na kutajwa kuwania tuzo mbalimbali duniani.
Yeye Maua, kwa kutambua ukubwa wake aliona ajipongeze kwa kujinunulia ndiga jipya aina ya Toyota Vanguard na kuliweka kado Toyota IST alilokuwa akilitumia awali.
MARIOO –BMWX1
Labda uwe mbishi tu juu ya mafanikio ya Maroo kwa mwaka 2021. Marioo ambaye amekiwasha vilivyo na Ngoma ya Mama Amina kisha Beer Tamu; kwa mafanikio hayo aliona naye ajinunulie gari la kifahari aina ya BMWX1.
NAY WA MITEGO -TOYOTA LAND CRUSER PRADO
Mara baada ya kutimiza umri wa miaka 33, Nay aliamua kujipa zawadi ya gari kutokana na mapambano yake ya kujitafutia maisha, hivyo akaamua kununua gari hilo aina ya Toyota Land Cruiser Prado.
Lakini katika mlolongo huo wa wasanii kujinunulia magari ya kifahari wapo walionunuliwa na kupewa kama zawadi na watu waliokaribu nao kutokana na sababu mbalimbali kama tutakavyoona hapa chini.
BABA LEVO –TOYOTA HARRIER
Baba Levo anaangukia kwenye lile fungu la walionunuliwa magari baada ya kupewa gari aina ya Toyota Harrier na msanii Diamond Platnumz.
Kwa mujibu wa Baba Levo, Diamond alimnunulia gari hilo lewnye thamani ya shilingi milioni 26.5.
Alisema Diamond alimnununulia gari hilo kutokana na kuwa mmoja wa wafanyakazi wake katika kituo chake cha radio. Baadaye walitoa wimbo wa pamoja wakiuita jina la Shusha na ambao ulifanya vizuri.
ANJELLA -TOYOTA CROWN
Mwanadada huyu wa Bongo Fleva alinunuliwa gari aina ya Toyota Crown na bosi wake ambaye Harmonize au Konde Boy Mjeshi.
Hii ilikuwa Julai 2021 ambapo Harmonize alisema amempa kama zawadi.
Anjella ni mmoja wa wasanii walio katika Lebo ya Konde Music Worldwide na alizawadiwa miezi sita tu baada ya kujiunga katika lebo hiyo ya Harmonize.
JOSE WA MIPANGO -TOYOTA CROWN
Harmonize alimzawadia jamaa yake Jose wa Mipango gari aina ya Toyota Crown. Harmonize alidai ametoka mbali na jamaa huyo ambaye ni miongoni mwa viongozi ndani ya Konde Gang Music Worldwide.
Inaelezwa kwamba hii ni mara ya pili kwa Harmonize kufanya hivyo kwani mwaka jana aliwahi kuwazawadia magari vijana wake, Ibraah na Country Wizzy.
KHADIJA KOPA – TOYOTA ALPHARD
Khadija Kopa ni Malkia wa Taarab Afrika ambaye alizawadiwa gari na mwanawe, Zuchu.
Gari hilo aina ya Toyota Alphard alizawadiwa baada ya Zuchu kupata mafanikio ya kimaisha akiwa ndani ya Lebo ya Wasafi Baby Classic (WCB) aliyojiunga nayo Aprili 8, 2021.
Kama utakumbuka mwaka juzi, Diamond alimzawadia Zuchu gari jipya aina ya Toyota Vanguard baada ya kufanya vema kwenye uzinduzi wa Extended Playlist (EP) yake aliyoiita I’m Zuchu katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar.
Makala; Elvan Stambuli, Bongo