
WHOZU ni miongoni mwa mastaa ambao ni zao la mitandao ya kijamii. Alijipatia umaarufu kupitia Instagram kwa aina yake ya uchekeshaji na hatimaye sasa ni staa wa Bongo Fleva.
Safari yake huwenda ikawa ndefu kuliko tunavyoweza kufikiria, lakini kitu cha kujifunza ni mafanikio yake kwa wakati huu ambapo tayari amefanikiwa kung’aa na ngoma zaidi ya 10 zikiwemo zake binafsi na zile alizoshirikishwa.
Aina yake ya uchekeshaji anayoitumia kwenye video za nyimbo zake na anazoshirikishwa zinatosha kueleza Whozu ana kipaji kama vile ambavyo Whozu aliwahi kusema kwenye moja ya intavyuu zake.
Kwa muda ambao jamii ilianza kumuelewa kupitia nyimbo zake kama Tunavesha na Huendi Mbinguni, Whozu alipata bahati ya kuchaguliwa kuwa balozi wa kampeni za Uber na TCRA.
Mbali na uimbaji, Whozu ni mwandishi wa ngoma mbalimbali na miongoni mwa ngoma alizoandika ni pamoja na Kiki Ni Gigi ya Gigy Money.
Unaweza kuuona uwezo mwingine ambao Whozu amebarikiwa na amefanikiwa kuuonesha.
Pongezi kwa wote waliomzunguka Whozu na kuhakikisha anazidi kusogea juu na kuwa chachu kwa vijana wa umri wake.
Hatua aliyofikia Whozu ni ile ya kujulikana kwa kila mtu hata asiyetumia Instagram hususan watoto na wazee.
Whozu hahitaji kujitambulisha kwa mtu yeyote, anaishi ndoto zake na anaonekana kufurahia na kupenda anachokifanya, ndiyo maana yupo hapo tunapomuona na kumsikia leo.
Whozu ni miongoni mwa vijana wa Kitanzania wa karne hii wenye nguvu na ushawishi mkubwa kwa vijana wa umri wake. Yote yasingewezekana kama Whozu angetumia Instagram yake kutafuta wasichana wazuri, aliamua kuwa bidhaa na kujiuza kwa wafuasi wake waliompa thamani na kumfanya athubutu kufanya vitu vikubwa zaidi.
Kuna namba kubwa ya vijana wenye umri wa Whozu wanatumia Instagram kutafuta warembo wakati wengine wanatafuta mawasiliano na watu wanaowashawishi.
Kama kijana unatumia Instagram kutengeneza namba ya wafuasi wasiokulipa na kutembelea DM za wasichana, jifunze kwa Whozu hutabaki kama ulivyo.
Jina lake halisi ni Oscar Lello, mbali na Tunavesha na Huendi Mbinguni, Whozu ametisha na ngoma nyingine kama Buku, Me Amore, Doko, Roboti, Mazoea na nyingine nyingi na kwa sasa anatamba na mkwaju mkali unaoendelea kukiwasha pale mjini YouTube unaokwenda kwa jina la Chawa.
Kama kawa, IJUMAA SHOWBIZ imefanya mahojiano maalum (exclusive) na Whozi ambaye anafunguka mambo kibwena;
IJUMAA SHOWBIZ: Mambo vipi Whozu?
WHOZU: Salama kabisa Mungu anasaidia, vipi za kazi?
IJUMAA SHOWBIZ: Salama kabisa kazi zinakwenda kama kawaida. Hongera kwa kuendelea kufanya mambo mazuri kwenye muziki wako…
WHOZU: Ahsante sana ila shukrani zangu zaidi ziende kwa mashabiki wangu maana bila wao mimi siyo kitu.
IJUMAA SHOWBIZ: Mwaka wa 2021 ulikuwaje na umejipangaje na huu hapa wa 2022?
WHOZU: Nimejipanga vyema sana kwa kweli.
IJUMAA SHOWBIZ: Unawaahidi kitu gani mashabiki wako?
WHOZU: Ninataka kuwaahidi mashabiki wangu mambo mazuri kabisa kwa mwaka 2022.
IJUMAA SHOWBIZ: Ila kuna kitu kinasemwa sana juu yako…
WHOZU: (anashangaa) kitu gani tena hicho?
IJUMAA SHOWBIZ: Mbona unashangaa, siyo ya wewe na Tunda maana hicho kinajulikana, mmeashaachana au? Lakini kuna lingine jipya…
WHOZU: Ndiyo uniambie ni jipya gani?
IJUMAA SHOWBIZ: Ni kuhusiana na wewe na msanii mwenzako, Badest…
WHOZU: Hapana, hilo sijasikia kabisa ndiyo kwanza nalisikia kwako.
IJUMAA SHOWBIZ: Mashabiki wanadai kwamba unamuiga Badest staili yake ya uimbaji na swaga zake, je, unajibu mapigo gani juu ya tuhuma hizo?
WHOZU: Kiukweli wananisingizia kabisa, mimi simuigi mtu kuimba, kila mtu anafanya staili yake ya uimbaji.
IJUMAA SHOWBIZ: Ndiyo mashabiki sasa wanadai hivyo kwamba ladha yako ya muziki haina tofauti kabisa na Badest.
WHOZU: Ndiyo nataka kuwaambia kuwa hawajui kutofautisha.
IJUMAA SHOWBIZ: Vipi kuhusu maduka ya Whozu Empire, nini kinaendelea?
WHOZU: Nashukuru Mungu kwa sasa biashara yangu inaendelea vizuri kabisa.
IJUMAA SHOWBIZ: Unawashauri nini wasanii wengine ambao huwa hawadumu kwenye biashara zao?
WHOZU: Mimi naona malengo ndiyo kila kitu katika kila jambo tunalolifanya. Ushauri wangu ni kwamba tuweke nia kwenye kila kitu tunachotaka kukifanya, tutafika mbali.
IJUMAA SHOWBIZ: Ni mafanikio gani makubwa ambayo umeyapata hadi sasa kupitia biashara yako?
WHOZU: Nisiwe muongo, mbali na muziki, biashara imenifikisha mbali sana kimaisha; yaani imenitoa sehemu moja kwenda nyingine.
IJUMAA SHOWBIZ: Baada ya kuachana na Tunda unatamani kuja kuwa na mwanamke wa aina gani hapo baadae?
WHOZU: Siwezi kuzungumza chochote.
IJUMAA SHOWBIZ: Zungumza chochote pengine anaweza akajitokeza wa aina unayomtaka na mkaendana.
WHOZU: Kiukweli natamani sana mwanamke ambaye atakuja kuwa na sifa kama za mama yangu. Mama yangu ni mwanamke ambaye anajitambua yeye ni nani na anafanya nini, lakini pia ni mama ambaye anajielewa. Kwa hiyo natamani sana mwanamke wangu aje kuwa na tabia kama za mama yangu kwa sababu naamini kila kitu kwenye maisha yangu kitakuwa chepesi.
IJUMAA SHOWBIZ: Kwa nini huwa unapenda kuimba sana ngoma za kuamsha popo (zilizochangamka)?
WHOZU: Ni kwa sababu napenda sana watu wachangamke na kuimba nyimbo hizo kwa sababu zina mashabiki wengi. Pia muda mwingine mbona nachanganya na za mapenzi jamani au hamuoni?
IJUMAA SHOWBIZ: Whozu asante kwa ushirikiano wako.
WHOZU: Asante pia karibu tena na tena.
Makala: Khadija Bakari, Bongo