×

Samia: Kama Humpendi Samia Mheshimu Mungu Wako – Video

RAIS Samia Suluhu Hassan, amewataka mawaziri na manaibu waziri aliyowateua hivi karibuni kufanya kazi kwa kushirikiana badala ya malumbano na kugombana badala ya kutimiza majukumu yao yaliyowaweka kwenye nyadhifa hizo.

 

Samia ameyasema hayo leo Januari 12, 2022 kwenye Mkutano wake Maalum na Mawaziri na Manaibu Waziri uliofanyika katika Ikulu ya Chamwino, Dodoma.

 

“Imekuwa kama maradhi, document za serikali tunazikuta mitandaoni, watu wanabishana huko mtu anaende kuchomoa document inapigwa picha inawekwa kwenye mtandao, kama mnabisha ushahidi ni huo, hii haipendezi na hakuna serikali inaendeshwa hivyo.

 

“Serikali inatoka kwenye ofisi zetu inaingia kwenye mitandao, kudhibiti siri za serikali, ziwe za siri ‘classified’ hata zile ambazo haziko ‘classified’, tunatakiwa mambo ya serikali yaishie ndani ya serikali

 

“Kama mwenzako ana tatizo, mwite kistaarabu, mweleze siyo kutukanana. Siyo njoo hapa wewe una 1, 2, 3 nitakwenda kumwambia mama, hapana rekebishaneni kwanza huko. Mkianza kutunishiana misuri na kutishana, hatuwezi kufika.

 

“Dunia hii, nchi inayoitwa Tanzania ni moja tu na wananchi ni sisi tu, kama kuijenga na kuibomoa ni sisi. Sisi tuliobahatika kuwa kwenye nafasi mbalimbali tuna wajibu mkubwa wa kuibeba hiyo nchi na wananchi wake, chochote kinachokwenda vibaya ni SISI.

 

“Taasisi ya URAIS, ni taasisi siyo MTU. Lazima mmoja wetu awe Rais na unakuja na mamlaka yake. Yoyote anayekuwa hapo anafanyia kazi taasisi na kama humpendi aliyepo, penda nchi yako, kama humpendi muheshimu Mungu kwani tunaambiwa mamlaka yanatoka kwa Mungu.

 

“Sijui mna maradhi gani ndugu zangu, Waziri na Naibu Waziri hawaelewani, Waziri na Katibu Mkuu mambo mbalimbali, hili mimi silielewi kwa sababu kila mtu yuko pale kwa ‘qualifications’ zake na ameonekana anaaminika na anaweza kufanya ile kazi.

 

“Waziri na Naibu wake migongano, mnagombaniana safari, ooh safari ilikuwa yangu anakwenda yeye mimi hanipi, wakati sekta ni kubwa, kila mtu akashika eneo lake mkafanya kazi, migongano yenu siielewi, wakati mwingine mnagombana kwa maslahi.

 

“Kuna Sekta kama Maji, Afya, Elimu, Umeme Vijijini tumezipa kipaumbele kutokana na kuwagusa moja kwa moja Wananchi.

“Kwenye utalii kuna ugawaji wa vitalu, Waziri anataka agawe vyake pengine keshapata fungu lake,Katibu Mkuu na yeye keshachukua la kwake, inakuwa vuta nikuvute, nimesema kwa mfano, sina hiyo kesi, huko nyuma yalishatokea, Mkenda anajua zaidi.

 

“Mara moja kwenye Baraza la Mawaziri nikasema, mimi ninajua kila Mbuzi hula kwa urefu wa kamba yake, lakini nikawaambia mbona mnakula sana?, mnavimbiwa, jipimieni kuna mambo yanafanyika ni kufuru,” amesema Rais Samia.

 

Leave a Comment