
AKIWA na miaka 21 tu Erling Braut Haaland anazidi kuitikisa dunia wakati huu akiwindwa na klabu kadhaa kubwa barani Ulaya.
Klabu kama Real Madrid, PSG, Manchester United, Barcelona na Chelsea zimeonyesha nia ya waziwazi kuinasa saini ya straika huyo ambaye anazidi kuweka rekodi tu ulimwenguni.
Wiki iliyopita straika huyo anayekipiga ndani ya Borussia Dortmund aliweka rekodi ya kuwa na mabao mengi zaidi kuliko idadi ya michezo ambayo amecheza.
Haaland aliweka rekodi hiyo baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 5-1 mbele ya SC Freiburg katika Dimba la Signal Iduna Park.
Mabao hayo mawioli yamemfanya straika huyo raia wa Norway kufikisha mabao 78 katika michezo 77 tangu aanze kuitumikia miamba hiyo ya Ujerumani katika mashindano yote.
Haaland alitua ndani ya Dortmund ndani ya msimu wa 2019–20 na kuanza kasi yake ya kutupia akimaliza na mabao 15 katika mechi 13 za Ligi Kuu ya Ujerumani ‘Bundesliga’ alizocheza kwa msimu huu. Jumla katika mashindano yote straika huyo alimaliza msimu huo akiwa na mabao 16 baada ya kucheza mechi 18.
Kama hiyo haitoshi msimu uliofata nyota huyo anayevaa jezi namba 9 ndani ya Dortmund msimu wa 2020–21 aliweka kambani mabao 27 katika mechi 28 ambazo alishuka dimbani ndani ya Bundesliga.
Kwa msimu huo alikuwa na kasi ya hatari ya kufunga mabao akifunga mabao 41 katika mechi 41 ambazo alishuka dimbani kwenye kikosi hicho kinachonolewa na kocha Marco Rose.
Msimu huu wa 2021–22 ukiwa ndiyo unaenda kufika kati straika huyo tayari ameshaonyesha kasi ya kutupia mabao akiwa amefunga mabao 15 katika mechi 13 ambazo amecheza tayari. Jumla katika mashindano yote hadi sasa amefunga mabao 21 katika mechi 18 ambazo ameshuka dimbani.
Mabao hayo yanamfanya Haaland kuwa na rekodi ya kufunga mabao 78 katika mechi 77 ambazo amecheza jumla akiwa na kikosi hicho cha Dortmund.
Ikumbukwe kuwa msimu huu Haaland haukuanza vizuri kwa kuwa alikumbwa na majeraha lakini aliporudi uwanjani bado akaonyesha yeye ni nani katika kuwatungua makipa.
Haaland amekuwa mshindani mkubwa wa mshambuliaji wa Bayern Munich, Robert Lewandowski katika kuwania kiatu cha ufungaji bora ndani ya Bundesliga. Tangu atue katika ligi hiyo Haaland ndiye amekuwa mshindani halisi wa mshambuliaji huyo raia wa Poland.
Kwa msimu huu wawili hao wanakimbizana katika msimamo huo wakati Lewandowski akiongoza na mabao 23, Haaland akiwa na mabao 15 katika nafasi ya tatu. Nafasi ya pili yupo Patrik Schick wa Bayer Leverkusen mwenye mabao 18.
Kwa mwenendo huo wa Haaland na kasi yake ya mabao ndani ya Dortmund imemfanya kuwa kipenzi cha mashabiki wengi wa timu hiyo tangu atue akitokea Red Bull Salzburg ya Austria.
Wengi wanatamani kuona mshambuliaji huyo atamalizaje msimu huu lakini hadi hapa alipofika inatosha kabisa kumtaja Haaland kuwa mashine halisi ya mabao.
DORTMUND, Ujerumani