
OMMY Dimpoz mzee wa Pozi kwa Pozi (PKP), alizaliwa na kupewa jina la Omari Nyembo lakini kutokana na kazi aliyoiachagua akaamua kujipa jina la Ommy Dimpoz, kisanaa Dimpoz ni zao la Top Band iliyokuwa chini ya msanii TID Mnyama au kama Warioba.
Dimpozi alianza muziki nyuma ya maiki ambapo alikuwa kama vocalist wa TID. Baada ya kupata uzoefu kidogo ikabidi ajaribu bahati yake na ndipo alipotoa ngoma inayojulikana kama Nai Nai. Nai nai ndiyo iliyomtambulisha kwenye Bongo Fleva.
Azidi Kupaa
Nai Nai ilikuwa ngoma ya Taifa iliimbwa na kila mtu na mafanikio hayo yakaweza kumtambulisha haraka Ommy Dimpoz katika kiwanda cha muziki nchini.
Wimbo huo ambayo alimshirikisha Alikiba iliweza kumpa tuzo ya msanii bora wa kiume anayechipukia katika tuzo za Kilimanjaro Music Awards. Dimpoz aliendelea vizuri na muziki wake ambapo alitoa ngoma zingine zilizokuwa moto. Vibao kama Baadae, Me and You alichomshirikisha Vanessa Mdee vikazidi kuing’ arisha nyota ya Ommy Dimpoz
Akafanikiwa kuwa kundi moja na wasanii ambao walikuwa wanaangaliwa kwa jicho la pekee Tanzania. Dimpozi kipindi chote rafiki yake mkubwa alikuwa ni Alikiba. Lakini baada ya Alikiba kutangaza kupumzika muziki ikabidi Dimpoz aunge urafiki na Diamond Platnumz ambapo walikuwa pamoja kila mahali.
Dimpoz alifanikiwa kuachia wimbo aliyomshirikisha J Martin. Wimbo huo ambayo ilipewa jina la Tupogo ukazidi kumpandisha chati Dimpoz na hata kumshauri rafiki yake Diamond atumie Saxophone kwenye nyimbo zake kama yeye alivyofanya kwenye Tupogo.
Agombana na Diamond
Baada ya muda kupita mahusiano ya urafiki wa Dimpoz na Diamond ukadorora na kila mtu kufanya yake na hata Alikiba aliporudi kwenye muziki ikabidi Dimpoz arudi tena kwa rafiki yake wa zamani. Walifanikiwa kutoa nyimbo za pamoja na Alikiba alimshawishi Dimpoz ajiunge na Lebel ya Rockstar4000. Dimpoz alijiunga na Rockstar 4000 ambapo mpaka leo amedumu nayo.
Augua ghafla akiwa Mombasa
Dimpoz akawa rafiki mkubwa wa Alikiba na hata Alikiba alipoenda kuoa nchini Kenya aliongozana na Dimpoz na hapo ndipo hadithi ya maisha ya Dimpoz ilipobadilika. Dimpoz akaumwa ghafla sauti ikawa inatoka na mikwaruzo na hapo ndipo alipopelekwa hospitali moja jijini Mombasa na baadae kupewa rufaa kwenda Afrika Kusini.
Apelekwa Afrika Kusini
Akiwa Afrika Kusini alipangiwa kufanyiwa oparesheni ya koo kwani hali yake haikuwa nzuri hata kidogo. Dimpoz alifanikiwa kutoka salama theatre na hali yake ikawa nafuu kidogo. Lakini siku chache kupita Dimpoz hali yake ikaanza kudorora tena hali iliyowalazimu madaktari wa Afrika Kusini kumuandikia rufaa ya kwenda Ujerumani kwa ajili ya matibabu makubwa zaidi.
Hali yazidi kuwa mbaya, Apelekwa rufaa ya kwenda Ujerumani
Baada ya uchunguzi ikabainika Dimpoz alikula kitu chenye sumu na kumsababishia kansa ya koo. Dimpoz akapelekwa nchini Ujerumani ambako alifanyiwa oparesheni na kubadilishwa mfumo mzima wa koo.
Dimpoz alipona vyema na kurudi nchini ila shukrani za dhati ni kwa Gavana wa Mombasa ambaye ndiye aliyegharamia matibabu yote ya Ommy Dimpoz kuanzia Afrika Kusini mpaka Ujerumani.
Apona kabisa na kumshukuru Mungu
Baada ya kurudi nchini Dimpoz alitoa nyimbo ya kumshukuru nyimbo ya kumshukuru Mungu. Nyimbo hiyo aliipa jina la ni wewe ndani yake akiwa ameandika mashairi ya kumshukuru Mungu kwa nafasi nyingine ya kuishi aliyompa. Dimpoz ameendelea na muziki ambapo ametoa vibao kadhaa vilivyomrudisha kwenye gemu kwa kishindo.
Amshirikisha Nandy kwenye nyimbo yake mpya
Nyimbo yake ya Kata aliyomshirikisha Nandy imefanikiwa kuziteka nyoyo za washabiki wa muziki nchini na ndani nje ya mipaka ya Tanzania. Hivi karibuni Ommy Dimpoz alipata dili la kuwa balozi wa GSM ambapo anatangaza bidhaa mbalimbali za GSM hasa bidhaa za mavazi.
Kwa sasa Dimpoz anatajwa kama msanii anayevaa vizuri zaidi na kupendeza kuliko msanii yoyote yule. wengine wamekuwa wakimpamanisha na Jux na Diamond Platnumz kwa kutupia pamba kali. Ana albam zake mbili Me N You, Ommy Dimpoz Chartbusters na ngoma kali za kutosha. Mungu azidi kukupa uhai na mafanikio makubwa Dimpoz.