×

Rais Samia: Jukumu la Mahakama ni Kutoa Haki – Video

Rais Samia Suluhu Hassan amesema jukumu la msingi la mahakama ni kutoa haki na katika utekelezaji wa jukumu hilo, mahakama zinapaswa kuzingatia sheria ili kutenda haki kwa wote bila kujali hali ya mtu kijamii au kiuchumi na kuongeza kuwa usimamizi na ufuatiliaji wa mahakama utaendelea kuimarika kutokana na matumizi ya mifumo ya Tehama katika mahakama zote nchini.

 

Rais Samia ameyasema hayo katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria yaliyofanyika katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma na kuwataka mahakimu na majaji, pamoja na kutumia vifungu vya sheria, wanapaswa kujiuliza ndani ya nafsi zao kama ni kweli wanatenda haki.

 

“Pamoja na kutumia vifungu vya sheria na ufundi mahakamani, kubwa kwa wewe unayetoa haki ni kusikiliza nafsi yako, je hapa natenda haki au sitendi haki. Lakini katika kutoa maamuzi utu wa mtu utazamwe.

 

“Na tunapozungumza utu wa mtu, ni yule unayemhukumu lakini na wewe unayetoa hukumu utu wako unakutumaje? Uchukue fedha unyime haki au umpe aliyetumia umahiri na ujuzi wa vifungu kumnyima haki mwenye haki, kwa hiyo utu ni muhiumu katika kutoa maamuzi yenu.

“Niendelee kusisitiza watendaji wa mahakama wenye dhima ya kuamua haki, kuendelea kufanya hivyo bila kufungwa sana na masharti ya kiufundi, nina maana gani? Kwamba mwananchi anapoleta kesi mahakamani hajui chochote, hajui apite njia gani, anategema mawakili,” amesema Rais Samia. 

 

Leave a Comment