
RAIS Samia Suluhu Hassan leo Jumatano, Februari 9, 2022 ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje Dodoma yenye urefu wa kilomita 112.3. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka amesema ujenzi huo utagharimu Sh bilioni 221 na utakamilika mwaka 2025.
Aliwaeleza waandishi wa habari jijini Dodoma jana kuwa, barabara hiyo itakayojengwa kwa kiwango cha lami itakuwa kiungo kwa barabara nyingine za jiji hilo. Kwa mujibu wa Mtaka, hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi huo itafanyika katika eneo la Makutupora-Veyula.
Barabara hiyo imegawanywa kwa wakandarasi wawili, M/s AVIC INTL Project na China Civil Engineering Construction Cooperation kutoka Jamhuri ya Watu wa China. Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Dodoma, Leonard Chimagu alisema barabara hiyo itajengwa kwa awamu mbili.
Alisema awamu ya kwanza itahusisha ujenzi wa kilomita 52.3 kupitia Nala, Veyula, Mtumba na Ihumwa na awamu ya pili itahusisha kilomita 60 kupitia Ihumwa, Matumbulu hadi Nala. Alisema barabara hiyo itafungua fursa za kiuchumi kwa wakazi wa Dodoma sanjari na kuondoa msongamano wa magari yanayokwenda mikoa mingine.
Rais wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), Dk Akinwumi Adesina anatarajiwa kuhudhuria tukio hilo la kuweka jiwe la msingi la barabara hiyo. Mwaka 2019 bodi ya benki hiyo iliidhinisha kutoa Dola za Marekani milioni 137.3 kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo.
Taarifa ya AfDB jana ilieleza kuwa, Tanzania inapiga hatua kubwa kwenye maendeleo ya miundombinu zikiwamo barabara. Mkurugenzi Mkuu wa AfDB kwa Afrika Mashariki, Nnenna Nwabufo alisema moja ya wajibu wao ni kuboresha maisha ya Watanzania hivyo benki hiyo itaendelea kuwa mshirika mwaminifu kwa Tanzania.