
MSHAMBULIAJI wa Yanga, Fiston Mayele, ambaye ndiye kinara wa utupiaji katika klabu hiyo akitupia sita,
amewaondoa presha mashabiki wa timu hiyo kwa kusema kuwa watulie kwani mambo mazuri yanakuja.
Hiyo imekuja mara baada ya Yanga kutoka suluhu dhidi ya Mbeya City katika mchezo uliopita wa ligi na hivyo kupunguzwa pointi dhidi ya watani zao, Simba kutoka 10 hadi tano.
Akizungumza na Championi Jumatano, Mayele alisema kuwa, kupata suluhu katika mchezo uliopita isiwe sababu ya mashabiki kuona watashindwa kuyatimiza malengo yao msimu huu ambayo ni ubingwa na kuahidikuwa bado watapambana kwa hali na mali kuhakikisha kuwa wanatimiza ahadi hiyo.

“Mashabiki wasiwe na wasiwasi na sisi kwani bado tupo katika mapambano ya kuhakikisha kuwa malengo yetu yatatimia msimu huu kuhakikisha kuwa tunatwaa ubingwa, hivyo wanatakiwa kutupa sapoti kila mara bila kuchoka ili tuendelee kusonga mbele.
“Michezo bado ni mingi sana kama ambavyo imeonekana na sisi kama wachezaji tunatakiwa kupambana bila kuchoka kwani kwenye nia pana njia siku zote na sisi tunayo nia kweli kuhakikisha kuwa mashabiki wanapata furaha ambayo wameikosa kwa muda mrefu,” alisema Mayele.
STORI: MARCO MZUMBE, DAR ES SALAAM