×

Ajinyonga Akituhumu Ndugu Wajomba Zake Kuua Ndugu Zake 16 Kishirikina

Williamu Mwalugelo (46) mkazi wa Kawajense Manispaa ya Mpanda amejinyonga kwa kutumia kamba ya manila kwa kujining’iniza kwenye dari chumbani kwake akituwatuhumu wajomba zake wawili kuua ndugu zake 16 kwa njia za ushirikina.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, ACP Ally Makame amethibitisha kutokea kifo hicho, akisema kabla ya hapo marehemu alikamatwa na Polisi kwa kosa la kusababisha taharuki katika eneo la Mpanda hoteli kutokana na vitu alivyokuwa amebeba vinavyoashiria ushirikina.

“Kweli tulimkamata tulipigiwa simu na wajomba zake amepeleka vitu vya kishirikina, aliwekewa dhamana, siku ya kupelekwa mahakamani aliomba ruhusa afuate mdhamana akaenda kujinyonga,” alisema Makame.

Mdogo wa marehemu, James Mwakapimba mkazi wa Mpandahoteli alisema tukio hilo linahusishwa na Imani za kishirikina na chanzo chake kinasababishwa na kugombania mali za urithi zilizoachwa na babu yao.

Mwakapimbe alisema usiku wa kuamkia Jumamosi ya Februari 12, 2022 kupitia ndoto marehemu alisikia sauti ya mama yake mzazi aliyekufa miaka mitatu iliyopita ikimtaka kufika makaburi ya Mwangaza.

“Ilimwambia ondoka nenda makaburini utakuta kuna kitu nitakuelekeza ambacho kimesababisha sisi wote tumekufa na sasa wanataka kuwaua ninyi watoto wetu,”amesema Mwakapimbe.

Alisema sauti hiyo ilimtaka afike nyumbani na achukue jembe aende kupalilia makaburi.

“Akaenda kwenye kaburi la mama yake akasikia sauti chimba, akaanza kuchimba akakata kitu kigumu akaambiwa hicho chicho, akakivuta huku nyuma anavutwa na watu hawaonekani hadi shati likachanika.

“Akatoa akakuta vyungu viwili vimebebanishwa ndani kulikuwa na fuvu la kondoo, pembe limefungwa na ushanga na vingine, akasikia sauti wapelekee kaka zangu ndiyo wenye mzigo huo,” amesema.

Aidha amesema aliweka kwenye mfuko akabeba kisha kupeleka dukani kwa mjomba wao John Mwakapimba lakini hakumkuta sauti hiyo ilimuelekeza kupeleka kwa mjomba mwingine.

“Alipofika aliweka aliweka chini akamwambia mzigo wako huu hapa utajua pa kuupeleka, watu walijaa kuangalia baadaye akarudi nyumbani. Baadaye alitokea rafiki wa wajomba zetu katufokea aliyewaambia kupeleka huo mzigo ni nani? Marehemu akapata hasira akampiga baadaye polisi walimkamata,” amesema.

Imedaiwa kuwa alikamatwa baada ya kushtakiwa na wajomba zake, wanafamilia walimuwekea dhamana Jumapili akatakiwa kuripoti polisi Jumatatu.

“Jana alienda kuripoti tukiwa naye kufika polisi wakadai anapelekwa mahakamani, akadai afuate fedha ya dhamana alichukua baiskeli baadaye tukapewa taarifa amejinyonga,” amesema.

Leave a Comment