
MWILI wa marehemu Dk. Mwele Ntuli Malecela umewasili jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo, majira ya saa sita na ndege ya KLM ukitokea jijini Geneva, Uswisi alikofikwa na mauti wakati akipatiwa matibabu.
Mwili umepokelewa na baba yake ambaye ni waziri mkuu mstaafu, Dk. John Samwel Malecela pamoja na waombolezaji wengi waliogubikwa na huzuni, waliokuwa wakiusubiri uwanjani hapo tangu majira ya jioni.
Baada ya kuwasili, msafara uliekea moja kwa moja nyumbani kwa mzee Malecela, See View jijini Dar es Salaam ambapo sala fupi ilifanyika.
Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Mama Kate Kamba, Mwenyekiti wa CCM Dar es Salaam, wameshiriki misa hiyo fupi ya kuupokea mwili nyumbani kwa mzee Malecela.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na ndugu wa marehemu, baada ya mwili kuwasili, ratiba itakuwa kama ifuatavyo:
– Jumamosi asubuhi, itafanyika sala fupi nyumbani kwa Dk. Malecela, Sea View.
– Baada ya sala fupi, mwili utaelekea Kanisa la Mtakatifu Albano ambapo utafanyiwa ibada kuanzia saa tatu hadi saa tano asubuhi.
– Baada ya kumalizika kwa misa, mwili utaelekea katika Ukumbi wa Karimjee kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho kwa watu wote pamoja na salamu mbalimbali za rambirambi kutoka kwa serikali, mashirika na wageni mbalimbali.
– Shughuli za Karimjee zinatarajiwa kumalizika saa kumi jioni kisha utapelekwa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, tayari kwa safari ya kuelekea Dodoma.
-Mwili unatarajiwa kuwasili Dodoma majira ya saa moja jioni ambapo moja kwa moja utapelekwa Hospitali ya Benjamin Mkapa kuhifadhiwa.
– Jumapili, waombolezaji wataendelea kuwasili nyumbani kwa Mzee Dk. John Malecela, Kilimani jijini Dodoma.
– Jumatatu, mwili utatolewa hospitali na kupelekwa nyumbani kwa Dk. Malecela, Kilimani jijini Dodoma majira ya saa nne asubuhi ambapo itafanyika sala fupi na baada ya hapo, mwili utaelekea Kanisa la Anglikana Dodoma.
Baada ya misa, mwili utapelekwa Mvumi kwa ajili ya ibada ya mazishi.