
SUPASTAA wa muziki nchini Tanzania, Diamond Platnumz anapambana na hali yake baada ya kuendelea kushambuliwa kutokana na video ya wimbo wake mpya wa Gidi kufanya vibaya kwenye Mtandao wa YouTube; tofauti na matarajio ya mashabiki wake ambao ni wengi.
Jumamosi iliyopita, Diamond au Mondi aliachia video ya wimbo huo, lakini ndani ya saa 24, ulishindwa kufikisha watazamaji milioni moja kama inavyotokea kwenye video zake mpya ambazo nyingine kama ile ya Waah ilipata zaidi ya watazamaji milioni moja ndani ya saa 10 tu tangu iachiwe kwenye YouTube.
Hii si kawaida hata kidogo kwa sababu nyimbo zote ambazo Diamond aliachia miaka mitatu iliyopita zilipata zaidi ya watazamaji milioni moja ndani ya saa 10 pekee. Hadi jana Jumapili, wimbo huo ulikuwa umepata watazamaji laki nane pekee.
Baadhi ya watu wanadai kwamba, hili ni anguko kubwa mno kwa Diamond na limesababisha mshtuko kwani kuna wasanii wameachia video zao hivi karibuni kama King Kiba, Harmonize na Zuchu ambao video zaidi zilipata watazamaji zaidi ya milioni moja ndani ya saa 24. Wengi wanaamini video nyingine kutoka kwa Diamond au Simba itafanya vizuri.
STORI; SIFAEL PAUL, DAR