
MSHAMBULIAJI tegemeo hivi sasa Yanga, Mkongomani Fiston Mayele, amesema kuwa malengo yao ni kucheza michuano ya kimataifa, mwakani baada ya msimu huu kuondolewa mapema huku wakiwaacha wapinzani wao Simba wakiendelea.
Yanga iliondolewa katika michuano hiyo katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo ilipata nafasi ya kucheza michuano hiyo baada ya Caf kutoa nafasi nne za ushiriki kimataifa baada ya Simba kufika hatua ya robo.
Timu hiyo msimu huu imeonekana kupania kucheza michuano hiyo mikubwa ya Afrika bila ya kubebwa na watani wao, Simba na badala yake kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Mayele amesema malengo yao lazima yatimie katika msimu huu ya kuchukua ubingwa ili wapate nafasi ya uwakilishi wa nchi kimataifa na hilo linawezekana kwao.
Aliongeza kuwa anaamini kwa kushirikiana na wachezaji wenzake, benchi la ufundi, uongozi na mashabiki ambao wanatoa sapoti kubwa uwanjani, watafanikisha malengo yao.
“Msimu uliopita tulipata nafasi ya kuiwakilisha nchi kimataifa, lakini tulishindwa kufanya vizuri kama walivyokuwa wenzetu (Simba), hivyo katika msimu huu tumepanga kuchukua ubingwa wa ligi ili tuwakilishe vizuri.
“Hivyo hatutaweza kupata nafasi ya uwakilishi kimataifa kama tusipochukua ubingwa wa ligi, hivyo niwatake mashabiki kuendelea kutusapoti uwanjani ili tufanikishe malengo yetu.
“Ninaamini mashabiki wa Yanga wana kiu ya kuona timu yao ikibeba ubingwa wa ligi msimu huu, hivyo waendelee kujitokeza uwanjani kama wanavyofanya,” alisema Mayele.
WILBERT MOLANDI,