
Urusi imekidhibiti kituo cha nishati cha nyuklia nchini Ukraine baada ya kukishambulia kwa makombora.
Moto ulizuka katika kituo cha nyuklia cha Zaporizhzhia – kikubwa zaidi barani Ulaya – na Ukraine imesema kuwa kilishambuliwa na wanajeshi wa Urusi.
Mamlaka imesema kituo hicho sasa kiko salama na viwango vya mionzi ni vya kawaida.
Viongozi wa dunia wameishutumu Urusi kwa kuhatarisha usalama wa bara zima, na rais wa Ukraine aliishutumu Urusi kwa “ugaidi wa kinyuklia”.

Rais wa Marekani Joe Biden aliitaka Moscow kusitisha shughuli zake za kijeshi katika eneo hilo, huku Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau akisema “mashambulizi ya kutisha” kutoka Urusi lazima yasitishwe mara moja.
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson alisema shambulio hilo “la kizembe” linaweza “kuhatarisha moja kwa moja usalama wa Ulaya yote”.
Viongozi wote watatu walizungumza na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kwa njia ya simu.
Bw Zelensky, wakati huohuo, alisema Urusi inataka kurudiwa kwa Chernobyl, eneo lililo shuhudia maafa mabaya zaidi ya nyuklia duniani mwaka 1986.
“Ikiwa kuna mlipuko, ni mwisho wa kila kitu. Mwisho wa Ulaya,”
Wizara ya ulinzi ya Urusi ililaumu shambulio hilo dhidi ya wavamizi wa Ukraine, ikilitaja kuwa “uchochezi mbaya” bila kutoa ushahidi.
Video kutoka kwa kiwanda cha nyuklia ulionyesha milipuko angani nyakati za usiku na kutoa moshi mwingi.