×

Ilibidi Nijaribu Upande Mwingine Kwa Mganga

 

BILA shaka ukiambiwa utaje listi ya mastaa wa kike wanaofanya vizuri kwenye uchekeshaji, huwezi kuacha jina la mwanamama Tatu Yusuph almaarufu Asha Boko.

 

Amepata umaarufu kupitia mwili wake mkubwa na jinsi anavyojua kucheza na kamera. Miongoni mwa filamu alizofanya vizuri ni pamoja na Kitimtim, Jazba, Back From New York na nyingine.

 

Gazeti la IJUMAA limefanya naye mahojiano kamili ambapo amefunguka mambo mengi kuhusu maisha yake; IJUMAA: Unahisi muonekanao wako ndiyo huwavutia madairekta wengi kiasi cha kutamani kufanya kazi na wewe kila mara?

 

ASHA BOKO: Nahisi hivyo pia kwa sababu watu wenye miili mikubwa kama yangu kwenye tasnia yetu ya sanaa ni wachache sana.

 

. IJUMAA: Kitu gani ambacho huwa unakizingatia sana pale unapokuwa mbele ya kamera?

 

ASHA BOKO: Kitu ambacho ninakizingatia mara nyingi nikutofanya kazi kizembe; yaani nikipewa kazi na mtu nahakikisha nimeifanya vizuri sana ili hata kesho na keshokutwa watu wakiiona wanasema kweli Asha Boko ameigiza.

 

IJUMAA: Ni jambo gani ambalo huwa ukiingia mtandaoni linakukera sana?

 

ASHA BOKO: Matusi, sipendi jinsi ambavyo watu wanatumia mitandao ya kijamii vibaya kwa kutukana na kuposti vitu visivyo na maadili, wakati inabidi tutumie mitandao vizuri kwa ajili yakujipatia riziki kama ambavyo wanafanya kina Shilole na wengineo.

 

. IJUMAA: Ni kitu gani ambacho huwa kinakukera sana kwa wasanii wenzako hasa wanawake na ungetamani kibadilishwe?

 

ASHA BOKO: Jambo la kwanza upendo, asilimia kubwa ya wasanii wa kike hatupendani kabisa, pia hata tukisaidiana tusianze kutangaziana, kwamba nilimsaidia mtu f’lani hiyo inakuwa siyo tabia nzuri, kama mmekosana ni bora mkakaa chini na kuyamaliza kwa sababu sisi wote ni ndugu.

 

IJUMAA: Umeshawahi kwenda kwa mganga?

 

ASHA BOKO: Nimeshawahi kwa nini nisiende bwana aah!

 

IJUMAA: Ulikwenda kwa lengo gani?

 

ASHA BOKO: Kuna kipindi wakati ndiyo nahamia Bagamoyo, niliumwa miguu nikasema inawezekana labda ni tatizo la mifupa kwa sababu ya unene, nikahangaika nikaenda hospitali nikapimwa kila kitu, lakini tatizo likawa halionekani. Nikasema wee msinitanie, ndiyo ikabidi nijaribu upande mwingine wa mganga, nashukuru Mungu nilitibiwa nikapona kabisa.

 

. IJUMAA: Ni zaidi ya mwaka sasa tangu uingie ndani ya ndoa na mwanaume mwingine baada ya mume wako wa kwanza kufariki, maisha ya ndoa ya sasa unayaonaje?

 

ASHA BOKO: Kwa kweli nisiwe muongo, maisha ya ndoa nayafurahia sana kwa sababu nimepata mume bora na mwenye upendo wa dhati kwangu.

 

IJUMAA: Wakati unaolewa kuna baadhi ya watu walidhani ile ndoa yenu ni kiki, una lipi la kuwaambia

 

ASHA BOKO: Wala siyo kiki, mimi niliolewa kweli na sasa tunakaribia kutimiza miaka miwili ya ndoa yetu

 

IJUMAA: Unawashauri nini wanawake wengine ambao wamekata tamaa kabisa ya kuolewa kutokana na umri wao kuwa mkubwa?

 

ASHA BOKO: Mwanaume akikupenda kweli hata uweje atakuoa tu, hivyo nawashauri wasikate tama, waendelee kuwa wavumilivu na wazidi kumuomba Mwenyezi Mungu bila kuchoka kila kitu kitakuwa sawa.

 

IJUMAA: Mpaka sasa una uzoefu wa kutosha kwenye ndoa, je, unawaambia nini wanawake ambao wapo kwenye ndoa kwa sasa?

 

ASHA BOKO: Unajua wanaume wanapambana sana kututafutia riziki wanawake hivyo kama mwanamke unatakiwa umpe heshima kwa sababu ndiyo kitu anachostahili, hivyo nawashauri wanawake wenzangu wawaheshimu sana waume zao hata kama amerudi usiku wa manane na akahitaji umfanyie jambo f’lani usinune wewe lifanye tu kwa sababu hujui alikotoka amekumbana na mambo mangapi.

 

IJUMAA: Unawaambia nini mashabiki wako?

 

ASHA BOKO: Nawapenda sana naomba waendelee kusapoti kazi zangu, pale wanapoona nimefanya vibaya wasisite kuniambia ukweli ili nizidi kujirekebisha kwa sababu lengo langu ni kuhakikisha nafanya kazi nzuri zaidi. Pia ndoa siyo ngumu jamani waolewe wasiogope.

Makala; Memorise Richard

Leave a Comment