
Viongozi wa Umoja wa Ulaya waliokutana nchini Ufaransa Alhamisi wamekataa kutimiza matakwa ya Ukraine ya kuingizwa haraka katika umoja huo, huku wakijadiliana kuhusu njia za kuisaidia nchi hiyo iliyovamiwa na Urusi.
Mataifa ya Umoja wa Ulaya yameungana kikamilifu kuunga mkono upinzani wa Ukraine, na kupitisha vikwazo vya kiuchumi visivyo na kifani dhidi ya Urusi katika muda wa wiki mbili zilizopita.
Lakini viongozi wamegawanyika kuhusu jinsi Brussels inaweza kuchukua hatua kwa haraka kuikubali Ukraine kama mwanachama, na jinsi jumuiya hiyo ya mataifa 27 inavyoweza kukata uhusiano wa nishati na Moscow.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy ameomba nchi yake ipatiwe uanachama wa haraka wa Umoja wa Ulaya kama uthibitisho wa kuungwa mkono na washirika wake wa Umoja wa Ulaya.
Makubaliano kuhusu hatua hiyo, hata hivyo, hayatafikiwa wakati wa mkutano wa kilele wa siku mbili unaofanyika katika kasri la Versailles magharibi mwa Paris, ambako rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alimkaribisha mwenzake wa Urusi Vladimir Putin mnamo 2017.
Baada ya masaa tisa ya mazungumzo ya mgogoro, wakuu wa nchi na serikali walimaliza siku ya kwanza ya majadiliano kwa makubaliano juu ya lugha inayotambua “shauku ya Ukraine ya kujiunga na Umoja wa Ulaya”, lakini waliacha kwenda mbali zaidi katika mchakato huo.
“Ilikuwa fursa ya kuonyesha uungwaji mkono usioyumba, thabiti kwa Ukraine, yaani, kujitolea kifedha, mali,” rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel alisema. “Ni wazi kwamba Ukraine ni mwanachama wa familia ya Ulaya na tunataka kuunga mkono juhudi zote za kuimarisha na kuunganisha uhusiano na Ukraine.”
Kwa sasa, Ukraine ina “Mkataba wa Ushirikiano” tu na Umoja wa Ulaya, ambao unalenga kufungua masoko ya Ukraine na kuileta karibu na Ulaya. Inajumuisha mapatano makubwa ya biashara huria na kusaidia kufanya uchumi wa Ukraine kuwa wa kisasa.
Jaribio la Ukraine la kupata uanachama wa haraka imepata uungwaji mkono wa hali ya juu kutoka nchi za Ulaya Mashariki, lakini maafisa wa Umoja wa Ulaya wamesisitiza kuwa mchakato huo unaweza kuchukua miaka, huku umoja kati ya wanachama wa sasa ukihitajika kuruhusu mgeni katika klabu hiyo.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema EU lazima itume “ishara kali” ya kuunga mkono Ukraine, lakini akafutilia mbali uwezekano wa nchi hiyo kujiunga na umoja huo hivi karibuni.
Waziri Mkuu wa Uholanzi Mark Rutte alisema alimuambia Zelenskyy kwamba kukubaliwa kwa Ukraine katika Umoja wa Ulaya hakuwezi kuharakishwa.