
HABARI njema kwa mashabiki wa Yanga ni kuwa mshambuliaji wao kipenzi, Mkongomani Fiston Mayele yupo fiti na amejumuishwa katika kikosi cha Mtunisia, Nasreddine Nabi kitakachowavaa wapinzani wao, KMC, Jumamosi ijayo.
Awali ilielezwa kuwa, mshambuliaji huyo anayetamba na staili yake ya kutetema mara baada ya kufunga bao, alipata majeraha makubwa katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu Bara waliocheza dhidi ya Geita Gold.
Mayele alishindwa kumalizia mchezo huo dhidi ya Geita baada ya kupata majeraha yaliyomsababishia atolewe dakika ya 70 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Daktari wa Viungo wa Yanga, Mtunisia Youssef Ammar, alisema kuwa Mayele hakupata majeraha makubwa yatakayomsababishia kuukosa mchezo ujao dhidi ya KMC.
Ammar alisema kuwa mshambuliaji huyo hakupata majeraha, lakini benchi la ufundi kwa pamoja walishauriana kumpumzisha kutokana na mahitaji ya mchezo unaofuatia dhidi ya KMC.
Aliongeza kuwa mshambuliaji huyo ndiye tegemeo hivi sasa katika kikosi cha Yanga, hivyo anahitaji uangalizi mkubwa kwa hofu ya kupata majeraha makubwa yatakayomsababishia kukaa nje ya uwanja muda mrefu huku mchango wake ukihitajika.
“Kati ya wachezaji wanaochezewa kwa kupaniwa ni Mayele, mabeki wa timu pinzani wote wanamuangalia yeye kutokana na kiwango bora cha kufunga mabao, hivyo ni lazima aongezewe ulinzi.
“Tulimtoa kwa makusudi katika dakika 70 ya mchezo wa ligi dhidi ya KMC baada ya kuona mabeki wa timu pinzani wanacheza kwa kumpania baada ya kumchezea rafu za makusudi.
“Hivyo mashabiki wa Yanga waondoe hofu kabisa, mchezaji wao yupo fiti na tayari kwa ajili ya mchezo ujao wa ligi dhidi ya KMC, ameanza mazoezi jana Jumanne asubuhi na wenzake gym,” alisema Ammar.
STORI NA WIRBERT MOLAND | GPL