
KOCHA Mkuu wa Simba, Mhispania Pablo Franco ameweka wazi kuwa ‘atawasapraizi’ wapinzani wake Berkane kwa kuingia katika mchezo huo na mbinu tofauti kabisa kulinganisha na zile walizotumia katika mchezo uliopigwa nchini Morocco.
Simba kesho Jumapili watashuka kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kuvaana na RS Berkane katika mchezo wao wa nne wa hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo mpaka sasa wamecheza michezo mitatu na kukusanya pointi nne.
Simba wana kumbukumbu mbaya ya kuchapwa na Berkane katika mechi ya kwanza kwa mabao 2-0 walipokuwa ugenini nchini Morocco Februari 27, mwaka huu.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Pablo alisema: “Mchezo utakuwa mgumu kutokana na ubora wa wapinzani ambao tunakwenda kukutana nao, lakini pia kutokana na namna msimamo wa kundi letu ulivyo, utakuwa mchezo wa maamuzi.
“Kama benchi la ufundi tumefanya tathmini ya ubora na mapungufu yetu na kuyarekebisha, nikuhakikishie kuwa tutaingia katika mchezo huu na staili tofauti ya uchezaji kulinganisha na mchezo wetu wa Morocco na ni lazima tuhakikishe tunatumia faida ya kuwa nyumbani kushinda mchezo huu.
Stori: Joel Thomas