
Makombora ya Urusi usiku wa Jumamosi yameipiga shule ya sanaa katika Mji wa Mariupol na kusababisha madhara makubwa ambapo watu takribani 400 walikuwa wamepewa hifadhi katika shule hiyo kufuatia mashambulizi makali yanayoendelea kwa muda mrefu nchini Ukraine kutoka kwa majeshi ya Urusi.
Kansela wa mji huo, kupitia Mtandao wa Telegram amethibitisha kutokea kwa mashambulizi hayo na kueleza kwamba bado haijafahamika ni watu wangapi wamepoteza maisha ingawa idadi kubwa ya watuw amefukiwa na kifusi.
Picha za satellite zinaonesha sehemu kubwa ya shule hiyo ikiwa imeharibiwa vibaya na mashambulizi ya anga yaliyofanywa na majeshi ya Urusi.

Tukio hilo linakuja siku chache baada ya tukio linguine kama hilo, ambapo ukumbi wa maonesho ya sanaa ulipigwa na makombora ya Urusi huku ndani yake kukiwa na watu takribani 800 waliokuwa wamepewa hifadhi ndani ya ukumbi huo.
Mji wa Mariupol ni miongoni mwa miji ya Ukraine iliyoharibiwa vibaya na mashambulizi ya Urusi kwa wiki kadhaa mfululizo ambapo huduma muhimu kama maji, chakula, umeme na madawa hazipatikani kutokana na mji huo kuzingirwa na majeshi ya Urusi.
Taarifa zinaeleza kwamba vikosi vya wanajeshi wa Urusi wanazidi kusonga mbele katika Mji wa Mariupol huku taarifa za Kiintelijensia zikieleza kwamba licha ya upinzani wanaoupata kutoka kwa majeshi ya Ukraine, huenda siku chache zijazo mji huo ukawa umetekwa kabisa na majeshi ya Urusi.
Video iliyokuwa na ujumbe kwa viongozi wa nchi za Magharibi uliothibitishwa na Shirika la Habari la Associated Press, umemuonyesha afisa mmoja wa polisi wa Mariupol akisema kwamba watoto na wazee wanafariki kwa wingi kutokana na mashambulizi ya Urusi katika mji huo.
Kutekwa kwa mji wa Mariupol itakuwa ni hatua kubwa ambayo imepigwa na wanajeshi wa Urusi katika vita hivyo, ukizingatia kwamba wamekuwa na wakati mgumu kupenya katika miji mikubwa, wiki tatu baada ya kuanza uvamizi huo.
Gazeti la New York Times limemnukuu mwanajeshi mmoja wa Ukraine akisema shambulizi la roketi limesababisha vifo vya hadi wanamaji 40 katika Mji wa Kusini wa Mykolaiv hapo jana.