×

The World You Left Behind – 45

Matumizi mabaya ya fedha za serikali na ubadhirifu mkubwa unaotokea kwenye Wizara ya Fedha, vinamsababishia waziri mwenye dhamana katika wizara hiyo, Abbas Magesa matatizo makubwa na kufanya roho yake iwindwe kwa udi na uvumba.

Mpango wa hatari wa kuyakatisha maisha yake unaandaliwa na kwa bahati nzuri, Grace, mwanamke aliyekutana naye kwenye mazingira ya kutatanisha, anamueleza kuhusu mpango huo na kumpa mbinu za nini cha kufanya ili kunusuru maisha yake.

Hatimaye siku ya tukio inawadia na kwa utaalamu wa hali ya juu, Grace anamuokoa Magesa huku watu wengine wote wakiamini kwamba waziri huyo amekufa kwenye ajali hiyo. Wawili hao wanatorokea mafichoni Mombasa, Kenya ambako Magesa analazimika kuanza maisha mapya kwenye ulimwengu mwingine tofauti kabisa.

Grace anasafiri kuelekea Israel kikazi na Magesa anaitumia nafasi hiyo kumpekua mwanamke huyo akitaka kuujua ukweli wa maisha yake. Anachokutana nacho kinamshangaza sana. Hatimaye Grace anarejea na Magesa anambana kwa maswali magumu, hali inayosababisha mwanamke huyo apasue jipu na kueleza ukweli.

Upande wa pili, uchunguzi wa kina juu ya kifo cha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG Mwampashi ambaye alikuwa na urafiki wa karibu na Magesa unazidi kushika kasi na viongozi wa juu wa usalama, wamepeana saa 72 kuhakikisha ukweli unafahamika kuhusu kilichojificha nyuma ya mauaji hayo na tayari kuna kila dalili ya siri kufichuka.

Grace na Magesa waliokuwa mafichoni Mombasa nchini Kenya, wanajiandaa kwa safari ya kuelekea sehemu ambayo Magesa haijui lakini wanapofika uwanja wa ndege, wanakutana na jambo linalomchanganya mno Magesa.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

“Your identities and passport please! (Vitambulisho vyenu na hati za kusafiria tafadhali) askari wa uhamiaji aliyekuwa pale mapokezi alisema kwa sauti iliyosikika vyema baada ya zamu ya Magesa na Grace kuwadia. Harakaharaka Grace akatoa vyote na kuviweka juu ya meza, yule askari akavichukua na kuvitazama kwa makini, kimoja baada ya kingine kisha akawakazia macho Magesa na Grace.

“Hebu ingieni ndani,” alisema askari huyo huku akiinua mkonga wa simu na kuanza kuzungumza na upande wa pili, Magesa na Grace wakabaki wakitazamana.
“Nakuomba usiongee chochote, niachie mimi kila kitu,” alisema Grace kwa sauti ya chini, Magesa akawa anatetemeka kwa hofu kwani hakujua nini itakuwa hatima yao. Grace akatangulia mbele na kuingia kwenye chumba walichoelekezwa huku Magesa naye akimfuata kwa nyuma.

“Hebu kaeni hapo,” alisema yule askari huku akinyoosha kidole kuwaonesha kwenye viti viwili vilivyokuwa ndani ya chumba hicho kidogo. Muda mfupi baadaye, maafisa wengine watatu waliokuwa wamevalia sare za askari wa uhamiaji wa Kenya waliingia na kuwazunguka.

“Hebu hivyo vitambulisho vyenu?” alisema yule askari aliyewaamuru kwa Kiswahili chenye lafudhi ya Kikenya kisha akarudia tena kwa Kiingereza. Alipopewa akawasogelea wenzake na kuanza kuwaonesha kitu kwenye vitambulisho hivyo.
“Can you please introduce yourselves so that we know exactly your where-abouts? (Mnaweza kujitambulisha vizuri ili tuelewe mnatoka wapi na mnakwenda wapi?” alihoji afisa mmoja aliyeonesha kuwa na mamlaka kuliko wenzake, akamuonesha ishara Magesa kwamba yeye ndiyo aanze kujitambulisha lakini Grace akaingilia kati.
“Mossad agent! ID code Bravo, Chali, Chali 761,” (Afisa wa Mossad! Namba ya utambulisho BCC761) alisema Grace huku akiingiza mkono mfukoni na kutoa medali ya chuma iliyokuwa na rangi za kipekee, wale askari wakapigwa na butwaa na kutazamana.
Kwa jinsi alivyojitambulisha, hawakuwa na wasiwasi kwamba mwanamke huyo alikuwa ni jasusi kutoka nchini Israel lakini kwa kuwa kazi zao zilikuwa zikihitaji zaidi uhakika, yule aliyeonekana kuwa kiongozi wao, aliipokea medali ile na kusogea pembeni kwenye mashine maalum, akaichomeka ile medali, picha kubwa ya Grace ikatokeza kwenye kompyuta ya kisasa iliyokuwa ndani ya chumba hicho.
Yule askari alitingisha kichwa kuonesha kukubaliana na alichokiona, wenzake nao wakatingisha vichwa kisha kwa pamoja wakampigia saluti Grace.
“How about your fellow madam!” (Vipi kuhusu huyu mwenzako?)
“A code red package in transit!” (Ni mtuhumiwa hatari, namsafirisha) alijibu Grace kwa lugha ya mafumbo ambayo haikuwa rahisi kwa mtu asiye mwanausalama kuielewa. Kwa muda wote huo, kijasho chembamba kilikuwa kikimtoka kwani hakuelewa ni mambo gani Grace alikuwa akizungumza nao.
Akashangaa wale maafisa wakipiga tena saluti kisha wakatoka na kumuacha yule wa awali aliyewaamuru kuingia ndani ya chumba hicho.
“Come with me!” (Nifuateni) alisema yule askari kwa unyenyekevu, Grace akampa ishara Magesa ya kumfuata, wakapita kwenye geti la pili bila kukaguliwa na kuingizwa kwenye mlango maalum wa VIP, yule askari akawasindikiza mpaka kwenye chumba maalum wanachotumia viongozi wa kiserikali au watu mashuhuri wanapokuwa uwanjani hapo, akainama kama ishara ya heshima na kuwaonesha sehemu ya kukaa kisha akageuza na kuondoka zake.
“Grace! Mbona sielewi kinachoendelea,” alisema Magesa kwa sauti ya chini huku wasiwasi mkubwa ukionesha kwenye uso wake. Grace akamtazama na kumuonesha ishara kwamba hatakiwi kuzungumza chochote mpaka watakapoingia ndani ya ndege.
Magesa akashusha pumzi ndefu na kugeuka huku na kule akiwa ni kama haamini kwamba hatimaye walikuwa huru, tena wakapewa na heshima juu ya kukaa kwenye sehemu ya watu mashuhuri.
Dakika kadhaa baadaye, sauti ya mhudumu wa kike wa uwanja huo ilisikika ikiwataarifu abiria waliokuwa wakitarajia kusafiri kwa ndege ya Shirika la Maldives Airline, Grace akamgeukia Magesa na kumpa ishara kwamba wainuke, akatii na muda mfupi baadaye, walikuwa wakipanda ngazi za kuingia ndani ya ndege hiyo kubwa.
“Usishtuke kwa kilichotokea, kama unakumbuka nilishakueleza kuwa mimi ni mpelelezi wa kimataifa ambaye nina uwezo wa kupita sehemu yoyote na kupewa heshima, hicho ndiyo kilichotokea pale.
“Ilibidi nijifanye wewe ni mtuhumiwa wangu na nakusafirisha kikazi ndiyo maana walituruhusu kwa urahisi,” alisema Grace kwa sauti ya chini huku akimsaidia Magesa kufunga mkanda wa siti yake, mwanaume huyo akakosa cha kujibu zaidi ya kushusha pumzi ndefu.
Kwa jinsi alivyokuwa anamchukulia Grace, kuanzia kipindi walichokuwa wakisoma pamoja, akifahamika kwa jina la Bertha Sapula, hakuwahi kudhani kwamba inaweza kutokea siku akawa mtu anayeheshimika kiasi hicho.
“Kwa hiyo tunaelekea wapi?” alihoji Magesa lakini kama ilivyokuwa mwanzo, mwanamke huyo hakumjibu chochote zaidi ya kuachia tabasamu pana na kurembua macho yake mazuri, akizionesha wazi hisia nzito za mapenzi alizokuwa nazo.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumanne ijayo kwenye gazeti hilihili.

Leave a Comment