×

Twanga Pepeta kufungua mwaka Dar Live

Ali Choki - Twanga_6 Na Mwandishi Wetu
BENDI kongwe ya muziki wa Dansi nchini, The African Stars International ‘Twanga Pepeta’ Januari 1 ambayo pia ni Sikukuu ya Mwaka Mpya, wanatarajiwa kufungua mwaka kwa kishindo ndani ya Uwanja wa Taifa wa Burudani, Dar Live uliopo Mbagala-Zakhem jijini Dar.

Ali Choki -Twanga_5Akizungumza na gazeti hili, Meneja wa Dar Live, Juma Mbizo alisema kuwa siku zote ukumbi huo hauishi kwa burudani na safari hii katika Sikukuu ya Mwaka Mpya wamewaandalia bendi isiyoshikika Bongo ya Twanga Pepeta ambayo italishusha sebene la kufa mtu mwanzo mwisho.

“Tunatarajia kufungua pazia la burudani kwa wakubwa kuanzia saa moja za usiku ambapo wapenzi wa burudani watapata kusikia ngoma zote za Twanga Pepeta zinazobamba kama vile Usiyaogope Maisha, Uso Chini na nyingine zinazotikisa hadi sasa,” alisema Mbizo.

Mbizo aliongeza kuwa usiku huo utaongozwa na vichwa hatari katika bendi hiyo ambavyo ni Luiza Mbutu, Ally Chocky, Rogart Hegga ‘Katapila’ pamoja na Msafiri Diouf ‘Lewandowsky’.

“Bila kusahau katika sikukuu hiyo, kutakuwa na burudani kwa watoto ambapo pazia la burudani litafunguliwa mapema kuanzia saa mbili za asubuhi na watoto watakutana na michezo mingi kama vile kuogelea, kubembea, kuteleza, kupanda ndege maalum na mingine mingi kutoka kwa kundi linalotikisa kwa mazingaombwe na sarakasi la Masai Warriors,” aliongeza Mbizo.

Leave a Comment