Ilipoishia wiki iliyopita
“Shule, wewe tulisoma wote primary,” msichana huyo alitoa jibu ambalo lilimchanganya Bata, kwani hakukumbuka kama amewahi kusoma shule.
Sasa endelea..
“Tumesoma wote, shule gani,” Bata aliuliza kwa shauku, akifahamu fika kuwa msichana huyo alikuwa amemfananisha.
Jully akatoa kicheko cha kuonesha ukweli wa anachokisema, halafu akampa simulizi ambayo Bata hakuwahi kuifikiria akilini mwake. Kuna wakati alisisimkwa mwili, lakini akajisikia vibaya msichana huyo alipomalizia kwa kumwambia;
“Kuna habari kuwa dada yako alifanya njama na mpenzi wake ili wakuue warithi mali, maana baada ya wewe kutoweka katika mazingira ya kutatanisha, waliuza mali zote na wenyewe wakahamia Afrika Kusini. Watu wote wanajua hivyo lakini walishindwa kuwafanya lolote kwa sababu ya kukosa ushahidi.”
Maelezo yale yalimchoma sana Bata, ambaye alilazimika kuwaeleza jinsi alivyookotwa porini akiwa hajitambui na wala hakuweza kukumbuka chochote katika maisha yake. Hadi anapewa simulizi ile bado nukta hazikuweza kuunga ili atambue jambo. Jully alipojaribu kumkumbusha baadhi ya matukio, ikiwa ni pamoja na uwezo wake wa kucheza mpira, kumbukumbu zikaanza kumrejea taratibu.
Bata akamuomba Jully amsaidie kufika katika nyumba waliyokuwa wanaishi na angalau kama anamfahamu ndugu yake yeyote ili aweze kupata sehemu ya kuanzia, kitu ambacho Jully alikubali lakini akimtahadharisha kuwa asingeweza kufuatana naye mbele za watu.
Bata aliweza kufika Bunju alikokuwa akiishi, ambako hata hivyo, hakuweza kumpata mtu yeyote anayemkumbuka, lakini mtu aliyenunua nyumba yao, alisema yapata wiki mbili zilizopita alimuona mpenzi wa dada yake, ingawa alisema alikuja mara moja akitokea Afrika Kusini anakoishi.
Habari zile zilimsisimua sana Bata, akaomba kama angeweza kupata mawasiliano yake. Jamaa hakuwa nayo, lakini akamuahidi kumtafutia. Wakabadilishana namba na yeye akaondoka, akiwa na furaha kubwa. Alihitaji kuonana na dada yake.
Tangu siku ya kwanza Bata alipopata habari zile, usingizi wake ulikuwa wa tabu sana, muda mwingi alikuwa akiwaza ni nini hasa sababu ya dada yake kushiriki katika nia ya kutaka kumuangamiza. Ni vipi mtu wa nje aliweza kumshawishi ashiriki kumuua ndugu yake?
Maisha yaliendelea na kasi ya uhusiano wake na Elina ilizidi kupamba moto. Pamoja na mawazo ya dada yake na mapenzi, lakini bado aliendelea kujituma katika kazi yake ya uuzaji mitumba. Alizidi kufahamika miongoni mwa wafanyakazi wa ofisi mbalimbali mjini, kutokana na uzuri wa nguo na viatu alivyokuwa akitembeza maofisini.
Elina, ambaye alisomea mapishi, alimshawishi Bata kumtafutia kisehemu kidogo ambacho angeweza kuuza vitu vya kupikwa kama vile maandazi, keki, chapati, viazi na vitu vingine vya aina hiyo.
Akamkubalia na katika kutafuta kwake, alifanikiwa kupata upande mmoja wa kontena lililokuwa limeegeshwa katika moja ya vichochoro maeneo ya Posta jijini Dar es Salaam, ambako msichana huyo alionesha umahiri wa kupika na kujikuta akipata wateja wengi.
Ili kunogesha eneo hilo la vinywaji baridi na vitafunwa, Bata pia alitumia nafasi hiyo kuweka viatu na nguo zake alizo ‘point’ kwa umakini mkubwa kutoka kwa wauzaji nguo na viatu maarufu wa mjini. Mchanganyiko huo ulilifanya eneo hilo kuwa na watu wengi karibu muda wote na hivyo kuwafanya vijana hao kuingiza pesa nzuri karibu kila siku ya kazi.
Siku moja wakati wakijiandaa kufunga eneo lao la biashara, macho ya Bata yakatua kwa mteja mmoja aliyekuja eneo hilo na kuomba apatiwe juisi na chipsi. Aliikumbuka sura hiyo, lakini akasahau ni wapi aliiona, akajitahidi sana kuvuta kumbukumbu zake, lakini hakuweza kubaini alikuwa ni nani.
Baada ya kujihangaisha sana, akakumbuka kuwa mtu huyo ni yule aliyemuona katika jengo moja mtaa wa Samora, miezi mingi iliyopita. Kitu kilichomsumbua akili Bata ni nani aliyekuwa mbele yake. Kwa kuona mtu huyo anaweza asimuone tena kabla hajamtambua, akapata wazo la kwenda kumuuliza, huenda atapata fununu za kujua ni nani.
Akainuka kutoka katika kiti alichokalia, akaingia ndani ya kontena, akaitega vizuri simu yake kabla ya kumpiga picha mbili tatu bila mwenyewe kujijua.
Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia sehemu inayofuata katika toleo lijalo.