
HATIMAYE uongozi wa Simba, kupitia kamati ya usajili umeamua kufanya kweli kwa beki wa Cape Town City ya Afrika Kusini, Nathan Idumba Fasika raia wa DR Congo ili aje kucheza pacha na Henock Inonga ambaye waliwahi kucheza pamoja huko nyuma.
Idumba alijunga na Cape Town City Julai 16, 2021 akitokea FC Saint Eloi ya kwao DR Congo, ambapo mkataba wake na Cape Town unatarajiwa kufikia kikomo Juni 30, 2026, ila historia yake inaelezwa kuwa amewahi kucheza na Inonga timu ya Taifa ya Congo.
Chanzo chetu kutoka Simba kimeliambia Championi Jumatano kwamba, Inonga ndiye amewaambia uongozi wa Simba kumfuatilia kwa karibu Idumba ili aweze kupata muafaka katika safu hiyo ya ulinzi ambayo kwa sasa ipo chini ya Pascal Wawa, Joash Onyango na Kenedy Juma.
Chanzo hicho kiliongeza kuwa uwezekano wa Wawa kuendelea kubaki Simba msimu ujao ni mdogo hivyo wameona watafute mbadala wake haraka na jina lililokuwa la kwanza kupendekezwa ni Idumba.
“Ndugu yangu mimi naomba nikwambie tu kwamba, tayari Simba imeamua kufanyia kazi kwa karibu zaidi suala la ulinzi ambapo tayari imefanikiwa kufanya mazungumzo na makubaliano ya karibu na klabu ya Cape Town City ya Afrika Kusini.
“Hapa ninapokwambia hadi muda huu, tayari uongozi umefanikiwa kukubaliana na uongozi wa timu yake na kama mambo hayatabadilika basi uhakika Idumba atatua nchini mapema tu mwishoni mwa msimu huu.
“Uongozi wa Cape Town umewataka viongozi wetu wa Simba kufanya makubaliano Idumba hasa katika masuala la mshahara na mambo mengine kwani tayari Cape Town wao watahakikisha endapo tutamalizana na Idumba basi watamuachia na sisi tutapata moja kwa moja pacha ya uhakika kati yake na Inonga maana wamewahi kucheza pamoja timu ya taifa na timu ya FC Saint Eloi ya kwao Congo,” kilisema chanzo hicho.
Championi lilimtafuta Meneja Mawasiliano na Habari Simba, Ahmed Ally kuzungumzia ishu hiyo alisema:
“Ishu za usajili kwa sasa ni mapema na tunaangalia zaidi ni namna gani tunapambana kushinda mechi yetu ya Jumapili dhidi ya lakini usajili ukifunguliwa tutaboresha eneo la ushambuliaji na ulinzi lakini kwa sasa siwezi kusema ni beki gani ila msimu ujao utakuwa wa maboresho makubwa, Wanasimba watafurahi,” alisema Ahmed.
STORI NA MUSA MTEJA | CHAMPIONI JUMATANO