×

Kijana Kutoka Congo Ang’ara Mashindano Makubwa Zaidi Ya Qur’an Afrika 2022 – Video

Thiame Bouna kutoka Congo Brazaville, ameibuka mshindi katika mashindano makubwa zaidi barani Afrika ya kusoma na kuhifadhi Quran Tukufu yaliyofanyika katika Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam leo, April 17, 2022.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi, ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika mashindano hayo ambapo amemkabidhi mshindi huyo mfano wa hundi ya shilingi milioni 20 kama zawadi kwa mshindi wa kwanza pamoja na cheti maalum cha ushiriki.

 

Mashindano hayo ambayo ni ya 22 yanayoandaliwa na kuratibiwa na Taasisi ya Al- hiqma Foundation chini ya usimamizi wa Sheikh Nurdin Kishk yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa huku Mgeni Rasmi akiwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ambaye amewakilishwa na Dk. Mwinyi.

 

Katika mashindano hayo jumla ya washiriki 22 kutoka nchi 22 za Afrika wameshiriki ambapo wamepatikana washindi saba, wa kwanza akiwa ni Thiame aliyepata alama 99.75.

 

Mshindi wa pili katika mashindano hayo ni Abdullah Sengo Muhamad kutoka Uganda ambaye amepata alama 99.58 na kuondoka na zawadi ya shilingi milioni 12 huku Yusuph Ishaq kutoka Nigeria aliyepata alama 99.33 akishika nafasi ya tatu na kuondoka na kitita cha shilingi milioni 7.5.

 

Washindi wengine ni Irakiza Ismail kutoka Rwanda aliyeshika nafasi ya nne kwa alama 99.16 na kushinda shilingi milioni 5 na mshindi wa tano ni Ebd El Hamid kutoka Mauritania aliyepata alama 99.15 na kushinda shilingi milioni 3.

Aidha, imetolewa zawadi kwa mshiriki mwenye umri mdogo zaidi katika mashindano hayo ambaye ni Umer Nuredin Kasim mwenye umri wa miaka 9 aliyepewa zawadi ya aliyepewa dola 500 za Kimarekani ambazo ni sawa na shilingi milioni 1.6 huku msomaji wa sauti nzuri akishinda Muhamed Ibrahim Ghonim kutoka nchini Misri ambaye naye ametunukiwa dola 500 za Kimarekani.

Leave a Comment