×

Mume Wangu Anaishi Mara ya Pili – 6

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
“Na kama unasema hivyo kwa sababu ya Daniel kuja nyumbani usiku jana na yule aliyesema amekurithi. Yule ni mmoja tu ila alitaka kutuchezea akiamini sisi hatuna akili.”

Mara, Tiaki alitokea, nikamuaga wifi kwamba tuchati kwa meseji.
“Vipi mama Kisu, naona ulikuwa unaongea na wifi yako?”
ENDELEA MWENYEWE SASA…

“He! Umejuaje wewe?” nilishtuka sana kumsikia akisema hivyo.

“Nikiwa nje nilikusikia ukisema wifi…wifi… nikajua unaongea na wifi yako. We’ unadhani nimejuaje shemeji?” aliniuliza.
“Ahaa! Hapo sawa, nilitaka kushangaa sana. Maana mh!”
“Umeogopa nini shemeji?”

“Niliogopa shemeji. Nikasema huyu shemeji Tiaki vipi tena?”
Alicheka sana, akasema inaonekana mimi nilimfikiria yeye ni jini. Nikamkatalia lakini kutoka moyoni nikasema ni kweli nilidhani wewe ni jini.

Safari iliendelea. Mazungumzo kati yangu na Tiaki aliyesema ni shemeji yangu aliwahi kuja nyumbani yakaendelea. Lakini nikakumbuka maneno ya wifi kwamba, Daniel naye alipanda lile gari. Nikasimama kidogo ili niangalie nyuma kama nitamwona shemeji Daniel. Lakini sikumwona!

“Kuna mtu unamcheki?” aliniuliza shemeji.
“Kuna shemeji yangu nimeambiwa amepanda hili gari, sasa ndiyo nataka kujua ni kweli au la!”
“Umepanda na shemeji yako lakini hujui au?”
“Sijui, si ndiyo nimepigiwa simu na wifi hapa kaniambia.”

Basi, tulikaa kimya, basi liliendelea na safari na karibu kila abiria alibaki kimya.
Sasa tukakaribia kufika mjini, Tiaki akaniambia atakuja nyumbani siku moja kunisalimia. Nikamwambia karibu sana.

Ni Tiaki ndiye aliyetangulia kushuka, nikafuata mimi kwenye kituo kikuu cha mabasi, Ubungo. Nikaenda nyumbani na ndugu zangu.

Lakini tulipofika tu nyumbani, ndugu yangu mmoja aliniuliza nilikuwa naongea nini na yule abiria niliyekaa naye. Nikamwambia alisema ananijua, aliwahi kuja hapa nyumbani enzi za marehemu.

“Kwani yule si alikuwa nyumbani siku ile ya kumaliza msiba?”
Nilimshangaa ndugu yangu huyo, nikamuuliza ametumia kigezo gani kusema Tiaki alikuwepo pale msibani, akasema nguo alizovaa siku ile msibani ndiyo zilezile na hata sura yake yeye hajaisahau.

“Ina maana wewe ulipomwona umejua ni Daniel?”
“Ndiyo, kwani wewe ulipokaa naye kwa muda wote huo hujajua yule ni Daniel?”
“Jamani jamani. Sijamjua na wala sikumwona kama ni Daniel. Yeye kasema anaitwa Tiaki. Sasa kama wewe ulimwona ni Daniel, ndiyo nashangaa sana.”

Nilibaki nina mawazo sana kuhusu Tiaki kuwa Daniel. Lakini kwa mbali nilikubaliana na madai ya ndugu yangu. Moyoni nikajiambia ni lazima nijiangalie sana kuhusu huyu mtu anaitwa Daniel.
* * *
Wiki moja ilipita, siku hiyo nikiwa nyumbani, giza likikaribia kuingia, nilisikia hodi, nikamwambia msichana wa kazi akamwangalie anayegonga. Aliporudi aliniambia:
“Dada ni mgeni wako, anaitwa Tiaki.”
“Mh! Mwambie apite.”

“Sawa dada.”
Tiaki aliingia ndani kama mwenyeji, akasema:
“Kumbe hili ua linaendelea kukua, unalimwagilia sana maji.”
“Ni kweli shemeji. Karibu sana,” nilisema.

Lakini nikamshangaa sana kukumbuka ua. Akanifanya nimwangalie mara mbilimbili kama kweli naweza kuikumbuka sura yake kuwa, kuna siku alishawahi kufika nyumbani, lakini wapi!

Alipokaa tu kwenye kochi sebuleni na baada ya salamu, akasema:
“Siku ile nilipokuja ulinitengea juisi ya ukwaji, niliipenda sana shemeji.”
“Ooh! Nikupe?”
“Nitashukuru sana.”

Wakati namwandalia juisi, nilijiuliza swali. Ni kweli huyu Tiaki aliwahi kuja nyumbani? Lakini kwenye eneo la juisi, mbona mume wangu ndiye alikuwa akipenda sana juisi ya ukwaju na ndiye kisa cha mimi kutengeneza juisi hiyo kila wakati.
Wakati anakunywa juisi, aliniangalia akasema:

“Siku ile nilipokuja shemeji, jamaa aliniwekea wimbo wa Bubu Hutaka Kusema, uliimbwa na Bendi ya DDC Mlimani Park. Bado upo?”
Nilishtuka sana, nikamwangalia kwa kumkazia macho, akaangalia pembeni huku akisema:

“Kama upo niwekee shemeji.”
Kilichonifanya nimwangalie sana ni kwamba, huo wimbo aliosema aliwekewa na mume wangu, ‘Bubu Hutaka Kusema’ mume wangu naye alikuwa akiupenda kupindukia, nikamshangaa sana huyu Tiaki.
“Shemeji,” nilimwita.

“Naam.”
“Mbona sikuelewi?”
“Kipi usichonielewa shemeji?”
Je, nini kiliendelea? Usikose kusoma wiki ijayo mkasa huu unaoitwa Mume Wangu Anaishi Mara ya Pili.

Leave a Comment