×

SIMULIZI YA KUSISIMUA: THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 21


MTUNZI: Hashim Aziz (Hashpower)
0719401968
ILIPOISHIA:
“Tunapoingia kazini, lazima mjue kwamba lengo letu siyo kuua watu wasio na hatia, kama tumetumwa mzigo fulani basi muhimu ni kuhakikisha mzigo unapatikana bila kusababisha vifo vya watu wasio na hatia, wananchi siyo adui zetu, adui zetu sisi ni polisi,” alisema, nikashtuka sana kusikia maneno hayo.

SASA ENDELEA…
Kumbe wakati wananchi wa kawaida wakiwaona polisi kama ndiyo watetezi wao, kwa upande wa wahalifu, polisi huwa ndiyo adui yao namba moja. Mamba alitufundisha kabisa kwamba tunapokuwa kwenye kazi, ukimuona polisi hakuna cha ‘msalia mtume’, ni lazima umuondoe vinginevyo yeye atakuondoa wewe.
Niliwafikiria polisi, nikauona ugumu wa kazi yao! Nikazifikiria familia zao, watoto wao, ndugu zao na kadhalika, nikajikuta nawaonea huruma sana.

Hata leo baada ya kupitia mambo mengi sana, ninachoweza kukisema ni kwamba miongoni mwa watu wanaofanya kazi kubwa sana na ambao serikali inatakiwa kuwafikiria sana kwenye suala la maslahi yao, ni polisi.
Nitakueleza baadaye matukio ambayo tulikuwa tukipambana na polisi na utakubaliana na mimi kwamba ni kazi ngumu sana inayohitaji wito na moyo wa kujitoa sana, unahatarisha maisha yako kwa ajili ya kuwalinda watu wengine na mali zao, unapambana na watu wanaofundishwa kwamba wewe ndiye adui yao namba moja! Inahitaji moyo sana.

Mafunzo yaliendelea kwa muda mrefu, ikafika zamu ya kuanza kufanya kwa vitendo kile tulichofundishwa. Wengi wetu tulikuwa na uwezo mdogo sana wa kulenga shabaha na kuna wakati nilimsikia Mamba akisema kwamba hawezi kujivunia kutufundisha kwa sababu anajua ndani ya siku chache tu, wote tutakufa.
“Mkikutana na polisi nyie hakuna atakayerudi hata mmoja! Lazima ujue kulenga siyo kufyatuafyatua tu risasi, mtakufa wote kama kuku,” alisema na kuanza upya kutuelekeza. Lilikuwa somo gumu lakini taratibu tulianza kuelewa, hasa kutokana na msisitizo aliokuwa anautoa.

Kingine nilichogundua ni kwamba kumbe kushika bunduki pekee hakuna maana kama hujui kulenga shabaha! Unaweza kuwa na bunduki na ukazidiwa ujanja na mtu mwenye mshale, cha muhimu zaidi ni kujua unapiga wapi na kwa sababu gani. Baada ya kujifunza shabaha, tulihamia kwenye mazoezi ya viungo, ‘mtiti’ ukawa ni zaidi ya jana yake.

“Wewe unakula nini! Mbona huliilii kama wenzako?” uzalendo ulimshinda Mamba na kuamua kuniuliza. Aliona kila zoezi analotoa, naenda naye sawa kwelikweli, sikumjibu kitu nikawa namtazama tu. Mbinu aliyonipa Bonta ilinisaidia sana. Siku hiyo ilipita, tukaendelea na mazoezi karibu kila siku kwa muda wa siku ishirini na moja.

Huwezi kuamini, baada ya kumaliza mafunzo hayo, tulikuwa ‘tumekwiva’ kwelikweli, hata siku niliyorudi nyumbani kwenda kuwasalimia na kuwapeleka fedha za matumizi, kila mtu alikuwa akinishangaa. Nilikuwa nimebadilika ghafla kutoka kwenye uvulana na kuingia kwenye uanaume.

Mwili wangu ulikuwa umejengeka vizuri kimazoezi, kifua kilikuwa kimepanuka, mikono imejaa na hata kutembea kwangu kulibadilika, nilikuwa kama ‘mjeshi’ flani hivi. Kule kuchekacheka nilikokuwa nao awali, kuliisha, muda mwingi nikawa niko ‘siriasi’ sana.

“Kwani umeingia jeshini nini mwanangu? Maana unatisha siku hizi,” mama aliniuliza, nikashindwa kujizuia kucheka, nikamdanganya kwamba mahali ninapofanya kazi, tunafanya kazi ngumu sana ndiyo maana nimebadilika, basi akawa ananishukuru sana kwa jinsi nilivyoweza kujitoa mhanga kwa ajili ya kumsaidia baba na kuisaidia familia yetu.

Aliniambia kwamba fedha ambazo nimekuwa nikiwatumia, zimesaidia sana kubadilisha maisha ya pale nyumbani na kwamba anajivunia kuwa na mtoto mwenye moyo wa uthubutu kama mimi.

Kuna wakati aliniambia wazi kwamba anajutia uamuzi wake wa mwanzo wa kunikataza kwenda mjini kwa sababu kama ningemsikiliza, tungeendelea kuzama kwenye umaskini na pengine tungempoteza baba mapema zaidi kwa kukosa fedha za kununua dawa na za matunzo.

Nilikuwa namuitikia tu mama lakini ndani ya moyo wangu nilikuwa najua ukweli wa kila kinachoendelea, na kama na yeye angekuwa anajua, kamwe asingeniruhusu nifanye nilichokuwa nakifanya. Basi nilikaa pale nyumbani mpaka mida ya kama saa sita za usiku, nikawaaga kwamba naondoka.

Kila mtu alishangaa na afadhali siku ile nyingine nilienda na Bonta mpaka pale nyumbani, wakawa wananiuliza nitaondokaje? Niliwajibu kwamba nimekuja na teksi ya rafiki yangu kutoka mjini na alikuwa ananisubiri stendi. Haikuwaingia akilini lakini mwisho hawakutaka kunikwaza hasa kutokanana mchango wangu nilioanza kuuonesha kwenye familia, nikaagana nao na kutoka.

Ni kweli nilikuwa nimekuja na teksi kutoka Dar es Salaam lakini nilimwambia dereva anisubiri pale stendi kwa sababu sikutaka niwe gumzo pale kijijini. Kusafiri na teksi kutoka Dar halikuwa jambo dogo. Basi nilienda mpaka stendi ambako nilimkuta dereva akiwa amelala kwenye siti yake, nikamuamsha na muda mfupi baadaye, safari ilianza.

Kwa mujibu wa sheria za bosi Mute, ilikuwa ni makosa kulala nje ya nyumbani kwako, kwa hiyo ilikuwa ni lazima nirudi mpaka Sinza, bila kujali nitafika saa ngapi. Tulisafiri mpaka Dar, yule dereva akanipeleka mpaka Buguruni kama tulivyokuwa yumekubaliana, nikamlipa fedha zake kisha nikapanda bodaboda mpaka nyumbani kwangu, Sinza.

Mpaka naingia ndani, ilikuwa ni karibu saa tisa za usiku, nikaoga na kwenda kulala maana asubuhi nilikuwa natakiwa kuwahi kazini. Nililala kidogo tu, alarm ya kwenye simu ikaniamsha maana niliitegesha iniamshe saa kumi na moja na nusu. Niliamka nikiwa mchovu, nikaenda kuoga na kuanza kujiandaa, nikaenda mpaka kazini.

“Leo kuna kazi usiku, bosi atawapa maelekezo,” aliniambia Bonta nilipoingia tu. Sikuwa najua ni kazi gani lakini moyoni nilijua kwamba kazi imeanza. Kweli mida ya kama saa nne hivi za asubuhi, Bosi Mute alituita kwenye chumba cha mikutano.

Kwa kawaida, alikuwa akiitisha kikao, watu wote wanaacha kila walichokuwa wanakifanya na kwenda kumsikiliza. Muda mfupi baadaye alikuja na kutangaza kwamba siku hiyo kutakuwa na kazi, akawataka watu wote wanaohusika na maandalizi kuhakikisha kila kitu kinakamilika haraka iwezekanavyo.

Watu wengi walionekana kumuelewa haraka, lakini mimi na wale wenzangu tuliomaliza mafunzo pamoja, tulikuwa gizani bado. Akawataka watu wote kutoka isipokuwa sisi ambao sasa tulikuwa tumebatizwa jina la Kikosi B.

Tulibaki tumekaa kwenye viti vyetu, watu wote walipotoka, akatutaka tusogee mbele kulikokuwa na kama ubao mdogo mweupe, akachukua ‘marker pen’ na kuanza kutuelekeza jambo. Kila mmoja akawa na shauku ya kusikia hiyo kazi inahusu nini?

“Leo saa kumi na mbili kwenye benki ya …(akaitaja jina), kuna mzigo utateremshwa. Mnatakiwa kuhakikisha tunaupata mzigo huo kwa gharama yoyote na kuufikisha kambini kwa sababu ni wa kwetu,” alisema, moyo wangu ukanilipuka paah!

“Tunaenda kuvamia benki?” nilijiuliza nikiwa ni kama siamini. Aliendelea kutuchorea mchongo mzima unavyotakiwa kufanyika, na akasema hatutaenda wote, bali watachaguliwa wachache kati yetu watakaoungana na Kikosi A kwa ajili ya kazi hiyo. Moyoni nikawa namuomba Mungu nisiwe miongoni mwa watakaochaguliwa.

“Kila mmoja akae tayari, muda wa kuondoka utakapofika mtatangaziwa waliochaguliwa,” alisema Bosi Mute wakati akikamilisha kutupa mchongo wa kazi hiyo. Aliondoka na kutuacha mle ndani, tukawa tunatazamana, kila mmoja akiwa kimya kabisa.

Basi baadaye tulitoka na kila mmoja akaendelea na kazi yake maana licha ya kazi hiyo, kila mtu alikuwa na kitengo chake, mimi nikaelekea kule kwenye kazi yangu ya kuosha magari. Kulikuwa na magari kama matatu hivi yaliyoingia jana yake, basi nikavaa nguo za kazi na kuanza kuyaosha huku mawazo kibao yakiendelea kupita ndani ya kichwa changu.

Ilipofika kama saa tisa hivi za mchana, magari mawili, Toyota Noah, yote yakiwa na rangi nyeusi na vioo vya tinted, yaliwasili na kuingia pale ndani. Nikaona pilikapilika zimeanza, nikajua sasa mambo yamewiva.

Kila mtu aliacha alichokuwa anakifanya na kuanza kuangalia ni nini kinachoendelea, nilimuona Bonta akiwakusanya wale wenzake ambao wote walikuwa wakubwa kwetu. Wakaingia kwenye chumba cha mikutano, sijui walikuwa wakijadiliana nini lakini muda mfupi baadaye, tulianza kuitwa mmojammoja.

Na mimi nilipoitwa, niliacha kila kitu na harakaharaka nikaelekea kwenye kile chumba cha mikutano huku mapigo ya moyo yakinienda mbio kwelikweli. Nilipofika, niliwakuta wenzangu watatu ambao tulikuwa pamoja kwenye Kikosi B, kwa hiyo na mimi nikawa wa nne.

“Mmechaguliwa na Bosi Mute kuungana na sisi,” alisema Bonta huku akitutazama, moyo ukanilipuka paah! Nikajua sasa mambo yamekwiva. Hakukuwa na muda wa kupoteza, wale watu wengine walitoka, mle ndani tukabaki sisi wanne, Bonta na wenzake watatu, kwa hiyo jumla tukawa nane.

Muda mfupi baadaye, yaliletwa masanduku mawili, yakawekwa pale mezani na Bonta akatuambia kila mmoja anatakiwa kuanza kujiandaa. Masanduku yalifunguliwa, la kwanza lilikuwa na nguo vikiwemo viatu kama vile wanavyovaa wanajeshi na makoti marefu meusi, na lile lingine lilikuwa na bunduki.

Tukaambiwa kila mtu achague vitu vinavyomfaa, tukawa tunatetemeka kwelikweli. Walianza akina Bonta, wakachukua vya kwao, ikafika zamu yetu. Hakukuwa na muda wa kupoteza, kwa hiyo kila mtu alichukua vitu vyake na tukaanza kubadilisha mlemle ndani kama tulivyokuwa tukipewa maelekezo.

Muda mfupi baadaye, kila mmoja alikuwa ameshavaa, kiukweli nguo hizo zilitubadilisha kabisa, sasa tukawa kwenye mwonekano wa kijambazi kwelikweli. Tulipewa pia kofia na miwani myeusi, baada ya kumaliza, Bosi Mute alikuja na kuanza kutukagua mmoja baada ya mwingine.

Ni kama alijua jinsi sisi ambao ndiyo ilikuwa mara yetu ya kwanza tulivyokuwa na hofu, akawa anatutoa hofu na kutuambia tunatakiwa kujiamini. Akaendelea kutupa mchoro wa jinsi kazi inavyotakiwa kufanyika na mwisho akatuambia kwamba Jombi ndiye atakayekuwa kiongozi wa msafara.

Sikuwa namjua sana huyo Jombi zaidi ya kuwa namuona mara mojamoja pale kambini. Alikuwa ni kipande cha mtu, amekwenda hewani halafu ‘amepasuka’ kwelikweli kutokana na mazoezi. Muda wote macho yake yalikuwa mekundu kama ‘nyanya’ na sikumbuki kama nimewahi kumuona akitabasamu au kucheka tangu nianze kumuona.

Kila mmoja alikabidhiwa bunduki yake, wale wakubwa wakachukua mbilimbili, bunduki kubwa na bastola, sisi tukapewa mojamoja. Baada ya hapo, tulitengeneza kama duara hivi, Bosi Mute akiwa katikati, akawa anaendelea kututoa hofu na kusisitiza kwamba anatuamini na hatuwezi kumuangusha.

Baada ya hapo, tulishikana mikono wote kwa pamoja kisha tukagongesheana ngumi na harakaharaka tulitoka kule nje, yale magari yalikuwa yamesogezwa mpaka mlangoni, tukaingia kwa makundi mawili, kila moja likiwa na mchanganyiko wa wakubwa wawili na wadogo wawili. Ukichanganya na madereva, kila gari lilikuwa na watu watano, safari ikaanza.

Tulitoka kwa mwendo wa kasi huku watu wote wakiwa wanatutazama, tukaingia barabarani na magari yakawa yanakimbia kwa kasi kubwa sana. Sikuwa nawajua madereva ni akina nani lakini walionesha kuwa ni wazoefu sana.
Safari yetu iliishia kwenye mtaa mmoja wenye pilikapilika nyingi, eneo ambalo baadaye nilikuja kulitambua kwamba ni Tandika. Tulisimama kwenye barabara ya vumbi ya mtaa huo, mita chache kutoka kwenye barabara ya lami.

Dakika chache baadaye, tuliona yale magari yanayotumika kubebea fedha na kuzisambaza kwenye benki mbalimbali, likipita kwenye barabara ya lami huku nyuma likiwa linasindikizwa na gari la polisi. Kwa wanaoyajua magari ya kubebea pesa watakuwa wanaelewa vizuri, lilikuwa ni kama Hiace ndogo lakini likiwa limezibwa pande zote.

Je, nini kitafuatia? Usikose kesho hapahapa! Kwa shilingi 6,000 tu unaweza kupata simulizi yote kwa mfumo wa softcopy, piga 0719401968. Pia ukitaka kusoma au kusikiliza hadithi nyingine kwa kuingia:

www.simulizizamajonzi7113.blogspot.com, Facebook: Simulizi za Majonzi au Youtube: Hashpower Online.

Usisahau kulike, share na ku-subscribe.

Leave a Comment