×

Mkali wa Hip Hop, Young Lunya Asaini Dili na Lebo ya Sony Music Entertainment Africa

Young Lunya maarufu kama Mbuzi akiwa ndani ya Studio

 

MKALI anayekua kwa kasi kwenye soko la muziki wa Hip Hop Afrika Mashariki, Young Lunya, amesainiwa rasmi na lebo kubwa ya muziki Afrika, Sony Music Entertainment Africa Family.

Young Lunya amefanya vizuri katika nyimbo alizoshirikishwa na wakongwe kama Professor Jay, Chidi Benz na Nikki Mbishi na alikuwa memba wa kundi maarufu la OMG kabla hajaachana nalo na kuwa solo artist mwaka 2019.
Alipoulizwa kuhusu dili la kusainiwa Sony Music Africa, Young Lunya amesema; “nimetokea kwenye mkoa ambao hata kuzungumzia lebo kubwa ni kama hadithi na ndoto lakini nilipambania kuzifanya ndoto zangu zitokee.

Young Lunya kwa sasa ndiye Rapa Bora Bongo

“Kwa kuona nipo kwenye moja ya lebo kubwa duniani naona ni baraka kutoka kwa Mungu na kuheshiwa. Nimejisikia furaha sana kusajiliwa Sony Music Entertainment kwa sababu wanawakilisha wasanii wakubwa ambao nawakubali kama ASAP Rocky, Future, Travis Scott na wengine kibao. Nawaahidi mashabiki wangu kwamba muda si mrefu Young Lunya atakuwa msanii wa kimataifa.”

Hivi karibuni, Young Lunya alishinda Msanii Bora wa Hip Hop wa Mwaka katika tuzo za Tanzania Music. Kwa sasa yupo mbioni kutoa albamu yake ya kwanza ambayo ndani yake kuna sauti za mastaa wakubwa Afrika kama Diamond Platnumz, Khaligraph Jones, Sho Madjozi na wengine kibao atakaowatangaza kadiri muda unavyosogea.

Mkuu wa Sony Music Africa Mashariki, Christine Mosha ‘Seven’ amemkaribisha kijana huyo mkali wa michano.
“Sina shaka na uwezo wa Young Lunya, ni zawadi ya kipekee na mtu mwenye vipaji vingi anayefanya vizuri kwenye gemu la Hip Hop na huu ni mwanzo mpya wa mapinduzi ya Hip Hop Afrika Mashariki,” alisema Seven.
Mkali huyo anatarajia kuachia singo yake ya kwanza inayokwenda kwa jina la vitu vingi Ijumaa ijayo Juni 10, 2022.

Leave a Comment