
JOKATE Urban Mwegelo; ni Mkuu wa Wilaya ya Temeke (DC) jijini Dar es Salaam ambaye ametoa tamko zito juu ya vishandu (wezi wanaoiba kwa kutumia pikipiki).
Jokate anasema kuwa, wahalifu hao wanaelekea kutokomea kabisa katika Wilaya yake baada ya kuimarika kwa ulinzi wilayani humo.
Jokate anavishukuru mno vyombo vya dola na sheria kwa kutokomeza uhalifu wa aina mbalimbali wilayani humo.
Jokate ametoa kauli hiyo alipokuwa akikabidhi pikipiki tano maalum na bora kwa ajili ya mambo ya ulinzi kwa Jeshi la Polisi Wilaya ya Temeke kutoka Kampuni ya Hero.

Jokate anasema kuwa, pikipiki hizo ni kwa ajili ya kufanya kazi za kiusalama maeneo mbalimbali wilayani Temeke.
“Naishukuru sana Kampuni ya Hero, wamejitahidi sana na vishandu sasa basi, maana pikipiki zina uwezo mkubwa sana wa kukimbizana na wahalifu,” anasema Jokate ambaye kabla ya kuhamishiwa Wilaya ya Temeke alihudu kwa ufanisi mkubwa kule wilayani Kisarawe katika Mkoa wa Pwani.
Vishandu ni jina lililopata umaarufu kwa vibaka wanaopora kwa kutumia pikipiki ambao hubebana wawili kwenye bodaboda ambapo anayekuwa amepakiwa nyuma ndiye hukwapua mikoba, simu na vitu vingine vya thamani kisha hutoka nduki kwa kumburuza anayekuwa amekwapuliwa na kumuachia majeraha makubwa mwilini.
CC; @sifaelpaul