×

Samia: Aibu Mkoa Wangu Kuwa wa Mwisho kwa Ufaulu

RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema hafurahishwi na matokeo ya mitihani ya taifa ya kidato cha nne na sita ya Shule za Zanzibar hasa Mkoa wa Kusini Unguja kwa kushika nafasi za mwisho.

Alisema ni aibu mkoa anaotoka Rais (Mkoa wa Kusini Unguja) kufanya vibaya katika mitihani ya taifa ikilinganishwa na mikoa mengine.

Aliyasema hayo jana wakati akizindua Taasisi ya Mwanamke Initiatives (MIF), visiwani hapo.

Aipongeza juhuzi za MIF na Serikali ya Zanzibar kwa kupania kuhakikisha wanapunguza tatizo la ufaulu mdogo visiwani humo.

“Kawaida mitihani inapomalizika, Wizara ya Elimu Tanzania huniletea mavitabu makubwa ya matokeo ya mitihani na flashi au CD ya kuonesha mitihani yote, na ninapoweka flash katika kompyuta yangu kwanza nakwenda katika Mkoa wa Kusini Unguja na ninapoona matokeo nashika kichwa…Mungu wangu ehee, nini hiki sasa, ni aibu, Rais wa Tanzania mkoa aliotoka upo mwisho,” alionyesha kusikitika Rais Samia.

Hata hivyo, alisema amevutiwa na maelezo ya Serikali ya Zanzibar kuhusu mabadiliko makubwa kukabiliana na changamoto hiyo ya ufaulu.

Aliyataja mabadiliko hayo kuwa ni uboreshaji wa mitaala ya kufundishia ili kutoa elimu yenye tija, kuweka kipaumbele kwenye mafunzo ya amali na kudhamiria kujenga shule 10 za mafunzo hayo, kuongeza shule za ufundi kila wilaya, na kuongeza ajira za walimu zaidi ya 4,000 kwa mwaka ujao wa fedha.

Alisema ni hatua kubwa na zinaleta matumaini ya kupunguza tatizo la ufaulu mdogo.

Aliitaka serikali kuajiri walimu wenye sifa, wa kujitolea ambao wameshaonyesha uwezo wao, pia kuwapima walioajiriwa na kuangalia wanaofanya vizuri na wasiofanya vizuri, waweze kujituma na kufundisha vizuri wanafunzi.

Aidha, alisema ili Zanzibar iwe na matokeo mazuri ya wanafunzi katika mitihani yao ya taifa ni lazima kuwapo ushirikiano kati ya wazazi, walimu na serikali huku akiwataka wazazi hao kufuatilia maendeleo ya elimu ya watoto wao.

“Changamoto ya elimu Zanzibar ni jukumu letu sote hatuna wa kumtupia lawama na ili wanafunzi wafaulu vizuri, jitihada za walimu, wazazi, sekta binafsi na serikali na wanafunzi wenyewe zinahitajika,” alisema.

Rais Samia alisema sio suluhisho mtoto anaposhindwa kufaulu kupewa mume, ni vyema kuwasomesha watoto wa kike na wakiume ili kwa pamoja wasonge mbele kimaendeleo.

Aliitaka jamii kushirikiana kuwalea watoto vizuri kwa sababu wasipowalea vizuri watazalisha watoto watukutu wanaojiingiza kwenye makundi yanayofanya vitendo viovu kwenye jamii.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah, alisema serikali itaendelea kuiunga mkono taasisi hiyo ambayo imekusudia kuboresha sekta ya elimu Tanzania.

Alisema maono ya taasisi hiyo yanafanana na ya serikali katika kutekeleza suala zima la utunzaji wa elimu Zanzibar na serikali ina mpango wa kujenga vyuo vya ufundi katika wilaya zote visiwani humo ili kuwasaidia vijana kupata fursa.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Muhammed Mussa, aliipongeza taasisi hiyo kwa jitihada zao za kuwakomboa vijana kitaaluma lengo likiwa kuleta maendeleo ya kijamii na taifa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa MIF, Wanu Hafidh Ameri, alisema changamoto za kijamii ni nyingi na zinahitaji nguvu za pamoja kuzitatua kwa kuamua kuunga mkono juhudi za serikali kusaidia kutatua changamoto hizo.

Alisema wameelekeza nguvu kubwa katika elimu, kwa kuwa ndiyo nyenzo muhimu itakayomsadia kijana husasan msichana kuendesha maisha yake na kuepuka udhalilishaji.

“Tunalenga kubadili maisha ya vijana waondokane na umaskini, tukielekeza nguvu kubwa za kuinua kiwango cha ufaulu na wale wenye utashi wapatiwe mafunzo ya ufundi nawaomba wadau wote watuunge mkono,” alisema Wanu.

Leave a Comment