×

Waziri Jafo Azindua PETCO Kuimarisha Ukusanyaji Plastiki na Kuzichakata

Waziri Selemani Jafo akizungumza kwenye uzinduzi huo.

 

 

Julai 2, 2022: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mh. Dk. Selemani Said Jafo amazindua rasmi kampuni iitwayo Polyethylene Terephthalate (PET) Recycle Company (T) Ltd (PETCO)  iliyoanzishwa na wadau wanane kwa ajili ya kuimarisha ukusanyaji wa plastiki na kuzichakata tena katika jitihada za kuhifadhi mazingira.

Wadau wakishuhudia uzinduzi huo.

 

 

Waziri aliwapongeza washirika hao kwa kuanzisha wazo la mpango huo murua mwaka 2018 na kuhakikisha kwamba vifungashio vyao si tishio kwa mazingira.

“Mmethibitisha kuwa washirika wanaowajibika, nasi kama serikali tunawaunga mkono kabisa katika mpango huu na tutafanya kazi kwa karibu na PETCO kuhakikisha unatekelezwa vyema kwa ustawi wa mazingira yetu,” akasema.

Mwenyekiti wa Bodi ya PETCO, Bw. Unguu Sulay

 

 

Aliongeza kwamba hatua hiyo mpya itazalisha ajira zaidi ya 5,000 kwa mwaka, hivyo kukuza uchumi, kwani hatua mbalimbali za PET zitahitaji watu tofauti kwa ajili ya kushughulikia michakato husika.

Mh. Jafo alitoa mwito kwa mashirika mengine kujiunga na waasisi hao ambao ni A-One Products & Bottles Ltd (MeTL), Coca Cola Kwanza Ltd, SBC Tanzania Ltd (Pepsi), Nyanza Bottling Co. Ltd, Bonite Bottlers Ltd, Sayona Drink, Cool Blue Pure Drinking Water na Silafrica Ltd katika kufanya mchakato huo uwe wa kudumu.

Tukio la uzinduzi.

 

 

“Nawapongeza ninyi washirika waasisi wanane kwa mpango huu mkubwa. Mmethibitisha jinsi mlivyo makini juu ya suala la mazingira na nina uhakika wengine watafuata nyayo zenu,” alisema na kuongeza kwamba fedha zilizotolewa na kampuni hizi kuwezesha mpango huo zitumiwe ipasavyo.

Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk. Mhandisi Samuel Mafwenga alisema kuwa baraza lake limekuwa likifanya kazi kwa karibu na PETCO tangu wazo hilo lilipopokelewa miaka minne iliyopita.

“Tutaendelea kufanya nao kazi mkono kwa mkono kuhakikisha kwamba malengio yanatimia na NEMC itabeba jukumu la uangalizi ili kuhakikisha utekelezaji mzuri wa mradi katika mchakato wote,” alisema.

Mwenyekiti wa Bodi ya PETCO, Bw. Unguu Sulay alisema kwamba wanachama hao waasisi tayari wametoa dola 100,000 za Marekani kwa ajili ya mradi huo.

“Fedha hizo zitatumika kwa ajili ya elimu inayoendelea kutolewa kwa walaji na umma, shughuli za uhamasishaji kwa ajili ya kukuza uwajibikaji katika kusimamia mazingira, na  kuhimiza ukusaji wa plastiki kwa ajili ya kuzichakata tena,” akasema.

Alisema wakiwa ni wazalishaji, wainguzaji na wafanyabiashara katika bidhaa za PET na vifungashio, wanawajibika na bidhaa hizo baada ya matumizi.

“Sekta ya plastiki za PET inakiri kwamba upo ulazima wa kutazama suala hili, hasa la hali ya vifungashio vya plastiki husika baada ya matumizi ni muhimu kulishughulikia ili kupunguza athari zake kwa mazingira,” akasema.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, mchakato huo utahusisha  wazalishaji wa malighafi, wachakataji wa bidhaa husika, wamiliki chapa, wauzaji rejareja, walaji na wachakataji upya pamoja na PETCO katika kutimiza wajibu kuhusiana na bidhaa za PET katika kile kijulikanacho kama Extended Producer Responsibility (EPR), inayohimiza kutazama suala la mazingira na gharama zinazohusiana, kwa ushiriki wa sekta binafsi.

Bw. Sulay alisema kuwa PETCO itawajibika kupata wachakataji upya wa plastiki hizo na kutoa ruzuku kwa ajili ya mikataba ya kuchakata bidhaa zote za PET nchini; kutengeneza bidhaa mpya zenye thamani (rPET); kusimamia masuala ya ukusanyaji ushuru kwa ajili ya  mipango ya ukusanyaji na uchakataji; kutoa elimu na kuwawezesha wakusanyaji na kuhimiza ukusanyaji na uchakataji kwa ujumla.

Hafla ya uzinduzi ilishuhudiwa pia na Rais wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanaznia (CTI), Leodgar Tenga na wadau wengine wa mazingira.

Leave a Comment