
WINGA wa klabu ya Barcelona ya nchini Hispania raia wa Ufaransa Ousmane Dembele anaripotiwa kukosa maandalizi ya msimu pamoja na vipimo vya afya wakati wachezaji wa timu hiyo wanaporejea leo kwa ajili ya safari ya maandalizi ya msimu mpya wa 2022/2023.
Dembele ambaye mkataba wake na Barcelona umemalizika bado yupo katika mazungumzo na klabu hiyo ya kuongeza mkataba mpya mara baada ya mkataba wake wa awali kumalizika.

Kocha wa Barcelona Xavi Hernandez alitoa maelekezo kuwa kama Dembele hawezi kukubaliana na mkataba mpya basi ataondolewa kwenye mipango ya klabu hiyo.
Hivi karibuni Rais wa Barcelona Joan Laporta ametamka kuwa Dembele anachotakiwa kufanya ni kitu kimoja tu kukubaliana na ofa iliyopo mezani au kukubali kuondoka ndani ya klabu hiyo.

Mkataba mpya aliopewa Dembele ni miaka mitatu (3) ambao unaambatana na punguzo la asilimia 40 katika mshahara wake, hiyo ndiyo ofa ya mwisho aliyopewa winga huyo wa zamani wa Borussia Dortmund ya Ujerumani.
Dembele ambaye kwa sasa hana timu amekuwa akiwaniwa na vilabu mbalimbali barani Ulaya vikiwemo Chelsea, Manchester United, Bayern Munich pamoja na PSG.