
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo kwa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kutumia eneo la Nanenane lililopo jijini Dodoma kwa ajili ya Ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa Miguu.
Rais Samia pia ametoa maelekezo hayohayo kwa Wizara kuangalia uwezekano wa kutumia eneo la Tanganyika Packers lililopo Kawe jijini Dar es Salaam kujenga Uwanja mwingine wa Mpira wa miguu kwa Jiji la Dar es Salaam ingawa amekiri kuwa eneo hilo linaweza kuwa na utata wa umiliki lakini amebainisha kuwa kama Serikali itaangalia jitihada za kutatua changamoito hiyo na hatimaye eneo litumike kwa ajili ya ujenzi huo.
“Kingine ni kuhusu ujenzi wa Access Sports Arena Dodoma najua mtatumia lile eneo la Nanenane ambapo ni pazuri, pakubwa na panafikika, Kwa Dar es Salaam inawezekana kwa kujenga kule Uwanja wa Mkapa ni mbali lakini mshauriane zaidi na Wizara ya Ardhi kuona juu ya kutumia eneo la Tanganyika Packers kama itawezekana kulitumia najua eneo lile lina mashaka kidogo lina Ownership za utata utata lakini tutaangalia Serikalini tukiona ule utata tunaweza tukauondosha basi litumike eneo lile kutengeneza hiyo Arena panafikika zaidi.” Alisema Rais Samia

Rais Samia ameyasema hayo wakati wa hafla ya kuipongeza timu ya wanawake ya Serengeti Girls chini ya miaka 17 iliyofanikiwa kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Dunia kwa Wanawake zinazotarajiwa kufanyika nchini India mwaka huu.
Aidha Rais Samia ametumia hafla hiyo kuwatakia kila lakheri klabu za Simba na Yanga juu ya maandalizi yao ya michezo ya kimataifa inayotarajiwa kuanza mapema baada ya kufunguliwa kwa msimu mpya wa 2022/2023