
KLABU ya Arsenal imempatia dili kiungo wake mshambuliaji wa zamani Jack Wilshare kuwa kocha wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 18.
Wilshare mwenyewe ambaye ni zao la kituo cha kukuzia vijana (Academy) cha Arsenal alipandishwa kwenye timu ya wakubwa mnamo mwaka 2008 na kufanikiwa kucheza zaidi ya michezo 197 ndani ya klabu hiyo kati ya mwaka 2008-2018.
Kiungo huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza ambaye pia alifanikiwa kuchezea klabu ya Bournemouth pamoja na Westham United zote za nchini Uingereza kwa muda wa miezi kadhaa iliyopita alikuwa akifanya kazi na timu ya vijana ya Arsenalkabla ya kupewa kandarasi rasmi ya kuwanoa vijana hao.
Baada ya kupewa kandarasi hiyo Wilshare alisema:

“Ni heshima kubwa kupewa nafasi hii, siyo siri kuwa naipenda hii klabu. Napenda kile tunachokifanya na mnajua wakati mzuri wa maisha yangu nimetumia katika klabu hii.
“Hii ni nafasi adhimu sana kwangu na nipo tayari. Nina njaa na siwezi kusubiri kuwasaidia vijana hawa kuwa bora ndani nan je ya uwanja.”

Katika kipindi chake cha miaka 10 alichohudumu ndani ya kikosi cha The Gunners alifanikiwa kushinda makombe mawili ya FA.