
TIMU ya Taifa ya Tanzania, inayonolewa na Kocha Mkuu, Kim Poulsen, jana iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Timu ya Taifa ya Somalia kwenye mchezo wa kwanza wa kuwania kufuzu CHAN 2023 uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar.
Bao pekee la ushindi lilipachikwa na kiungo mshambuliaji Abdul Suleiman ‘Sopu’ dakika ya 46 akiunganisha krosi iliyopigwa na Kibwana Shomari. Sopu bao lake hilo katika kipindi cha pili lilidumu mpaka mwisho wa mchezo huo na kuwatanguliza hatua moja Taifa Stars kwenye kusonga mbele katika mchezo ujao dhidi ya Uganda
Baada ya mchezo huo wa jana, timu hizo zinatarajiwa kurudiana Julai 30, mwaka huu uwanjani hapo ambapo mshindi wa jumla atakwenda hatua ya pili kucheza dhidi ya Uganda. Katika mchezo wa jana, kipa wa Taifa Stars, Aishi Manula alipata maumivu dakika ya 87, akatolewa uwanjani na nafasi yake ilichukuliwa na kipa Aboutwalib Mshery.
Ikumbukwe kuwa, michuano hiyo ya CHAN inatarajiwa kufanyika kuanzia Januari 8 hadi 31, 2023 nchini Algeria. Kama Taifa Stars itafuzu michuano hiyo, itakuwa ni mara ya pili kushiriki baada ya awali kucheza mwaka 2009 wakati timu ikiwa chini ya Kocha Mkuu, Marcio Maximo raia wa Brazil, michuano iliyofanyika Ivory Coast.